Brown Mauzo afunguka hisia zake baada ya mkewe Vera kufurahia wimbo wa ex wake, Otile Brown

Mauzo pia alipuuzilia mbali madai ya kutengana na mwanasosholaiti huyo ambayo yameibuka katika siku za hivi majuzi.

Muhtasari

•Mauzo ameweka wazi kuwa hakuna tatizo kwa mkewe Vera Sidika kufurahia nyimbo za aliyekuwa mpenzi wake, Otile Brown.

•Mwimbaji huyo  alidokeza kuwa kumezuka kutoelewana katika siku za nyuma, sawa na katika ndoa nyingine za kawaida.

Vera Sidika na Brown Mauzo
Image: Vera Sidika Instagram

Mwanamuziki mzaliwa wa Pwani Fredrick Mutinda almaarufu Brown Mauzo ameweka wazi kuwa hakuna tatizo kwa mkewe Vera Sidika kufurahia nyimbo za aliyekuwa mpenzi wake, Otile Brown.

Hii ni baada ya mwanasosholaiti huyo maarufu hivi majuzi kuchapisha video yake akisikiliza wimbo wa Otile Brown ‘Chaguo la Moyo’ na hata kuimba pamoja, hatua iliyovutia hisia mseto kutoka kwa wanamitandao Wakenya.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, Mauzo alibainisha kuwa hata yeye aliwahi kuchapisha wimbo wa mwanamuziki huyo mwenzake katika siku za nyuma.

“Haina tatizo, mimi nishaweka, ata mimi nishaweka. Haina noma, sote ni industry moja,” alisema Brown Mauzo.

Mauzo aliweka wazi kuwa suala la mkewe kufurahia wimbo wa Otile Brown haikumfanya ajisikie vibaya hata kidogo.

“Mimi sioni ikiwa tatizo kwa sababu, ukipenda wimbo utasema kwa sababu mtu wamchukia uchukie wimbo? Hata ya adui yako waweza kusikiza tena ukaipenda,” Mauzo alisema.

Aliongeza, “Hata kuongea wakaongea haina maana kwa sababu watu wanakua. Mambo yanapita nyuma na tunaepusha ile hakuna uhasama.”

Katika mahojiano hayo msanii huyo mzaliwa wa pwani pia aliweka wazi kuwa ndoa yake na mwanasosholaiti Vera Sidika bado iko sawa.

Brown alipuuzilia mbali madai ya kutengana na mama huyo wa watoto wake wawili ambayo yameibuka katika siku za hivi majuzi na kufichua kuwa uhusiano wao bado ni mzuri.

“Tuko poa, tuko poa. Tuko pamoja, kwani shida iko wapi. Hatujaachana, kwani tuliachana lini. Siwezi kudanganya, mimi Muislamu,” alisema.

Mwimbaji huyo hata hivyo alidokeza kuwa kumezuka kutoelewana katika siku za nyuma, sawa na katika ndoa nyingine za kawaida.

“Maisha huwa na changamoto, mahusiano ni safari nyingine ya pandashuka. Sisi sio wakamilifu,” alisema.

Katika wiki kadhaa zilizopita, wasiwasi mwingi umeibuliwa kuhusu hali ya ndoa ya wazazi-wenza hao wawili.

Hii inafuatia vitendo vyao hivi majuzi kwenye mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na kchapisha jumbe za mafumbo na hata kufuta picha.