"Chagua sura, hata wenye sura mbaya hu'cheat" Ex wa Stivo Simple Boy, Pritty Vishy afoka

Mrembo huyo mwenye umri wa miaka 22 alidokeza kuwa wanaume hu’cheat bila kujali sura zao.

Muhtasari

•"Kumbusho tu, chagua sura, hata wenye sura mbaya hu’cheat," Pritty Vishy alisema siku ya Jumapili.

•Siku za hivi majuzi, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 21 ameonekana kuzama kwenye huba nzito na mcheza santuri wa Kenya ambaye anaishi Marekani.

Image: INSTAGRAM// PRITTY VISHY

Mpenzi wa zamani wa mwimbaji Stivo Simple Boy, Pritty Vishy amewashauri wanawake kuzingatia sura wanapochagua mwanaume wa kuchumbiana naye.

Katika taarifa aliyoichapisha kwenye Instastori zake, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 22 alidokeza kuwa wanaume hu’cheat bila kujali sura zao.

"Kumbusho tu, chagua sura, hata wenye sura mbaya hu’cheat," Pritty Vishy alisema siku ya Jumapili.

Kauli hiyo ilikuja muda mfupi baada ya kipusa huyo kutupa vijembe kufuatia ufichuzi wa mke wa sasa wa Stivo kuhusu matatizo yanayomkabili msanii huyo kutoka Kibera.

Siku ya Jumamosi, Vishy aliwakumbusha Wakenya kwamba aliwahi kufichua matatizo mwimbaji huyo anakabiliana nayo lakini hakuna aliyemwamini.

Huku akitoa maoni baada ya mke wa sasa wa rapa huyo, Grace Atieno kufunguka kuhusu matatizo ya kifedha na usimamizi ambayo mwimbaji huyo anakabiliana nayo, Vishy alibainisha kuwa watu walidhani kwamba bado alikuwa amekwama kwake baada ya kujaribu kufichua tishio hilo.

Wakati huo huo, alionekana kuirushia vijembe ndoa ya sasa ya mwimbaji huyo kutoka Kibra akiashiria kuwa yeye ndiye alikuwa mshirika bora kwake.

“Nilisema lakini wote mlisema sijasonga mbele na maisha yangu. Sasa tuone. Somo lililopo ukiwa na mwanamke sahihi kando yako, mthamini kila mara na uwe na shukrani,” Pritty Vishy alisema kwenye Instagram.

Hii ilikuwa baada ya mkewe Stivo, Bi Grace Atieno kufunguka kuhusu masaibu ambayo yeye na msanii huyo wanapitia nyumbani.

Pritty Vishy na Stivo Simple Boy walidaiwa kuachana zaidi ya mwaka mmoja uliopita baada ya kuwa kwenye mahusiano kwa muda.

Siku za hivi majuzi, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 21 ameonekana kuzama kwenye huba nzito na mcheza santuri wa Kenya ambaye anaishi Marekani.

Wiki chache zilizopita, alichapisha picha za mcheza santuri  anayefahamika kwa jina DJ Starvy na kunukuu kwa maneno matamu kwake.

Ninapenda kila kitu kuhusu wewe. Unafanya kila kitu kizuri. Unajua unanifanya kichaa, sawa? Nakupenda babe @dj_starvy," alisema.

Starvy alijibu kwa kumhakikishia kipusa huyo mwenye umri wa miaka 21 kuhusu mapenzi yake makubwa kwake.

"Unajua nakupenda mama watoto," alisema.

Vishy aliendelea, "Nakupea watoto  8 mapacha ndani na kadhalika."

Kwenye Instastori, mpenzi huyo wa zamani wa Simple Boy aliendelea kukikiri jinsi mpenziwe mpya anavyomkosesha usingizi.

"Ni wangu wa pekee," alisema.

Starvy pia alimtambulisha Vishy kama mpenzi wake kwenye ukurasa wake na akamshukuru kwa kukubali kufichua uhusiano wao.