"Imetosha!" Amira adai talaka baada ya Jamal Rohosafi kutakia Amber Ray kheri za kuzaliwa

Muhtasari

•Jimal amepakia video yenye picha za mwanasoshalaiti huyo na kuambatanisha na ujumbe "Kheri za kuzaliwa, uwe na sherehe nzuri leo @iam_amberay" 

•Amira ameapa kwamba hatakubali tena kukosewa heshima tena huku akisema kuwa imetosha sasa anataka talaka.

•Amira amesema ameshindwa kustahimili tena huku akielewa kuwa leo ndio amepata ujasiri wa  kuacha yale ambayo yamekuwa yakimvuta nyuma.

Image: INSTAGRAM

Ama kweli walivyosema wahenga sikio la kufa halisikii dawa. 

Miezi michache tu baada ya mfanyibiashara mashuhuri Jimal Marlow Rohosafi kuanza kurejesha hali ya utulivu kwa ndoa yake, ni dhahiri kuwa hakupata funzo kutokana na kashfa iliyokuwa imeitikisa ndoa hiyo mapema mwaka huu.

Hivi leo mwanasoshalaiti Faith Makau almaarufu kama Amber Ray, ambaye kwa kipindi cha miezi kadhaa alikuwa mke wa pili wa mfanyibiashara huyo anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Jimal ametumia ukurasa wake wa Instagram kutakia mpenzi huyo wake wa zamani heri za kuzaliwa.

Baba huyo wa wavulana wawili amepakia video yenye picha za mwanasoshalaiti huyo na kuambatanisha na ujumbe "Kheri za kuzaliwa, uwe na sherehe nzuri leo @iam_amberay" 

Hatua hiyo hata hivyo haijapokewa vizuri na mama ya watoto wake wawili, Amira Marlow ambaye vile vile ametumia ukurasa wake wa Instagram kuonyesha ghadhabu yake.

Amira ameapa kwamba hatakubali tena kukosewa heshima tena huku akisema kuwa imetosha sasa anataka talaka.

"Kutoka leo tafadhali mnichukulie kama single mum. @jimal_rohosafi tayarisha karatasi ya talaka. Sitakubali unikosee heshima tena!!" Amira ameapa.

Amira amesema ameshindwa kustahimili tena huku akielewa kuwa leo ndio amepata ujasiri wa  kuacha yale ambayo yamekuwa yakimvuta nyuma.

Ametangaza kuwa kwa sasa atazingatia kulea watoto na kuendeleza biashara yake huku akilenga kusonga mbele na maisha yake.

"Leo tarehe 4 Novemba nimepata ujasiri wa kujisimamia. Ni hatua ambayo nilifaa kupiga kitambo lakini sikuwa na ujasiri. Lakini inafika wakati  ambapo unasema imetosha! Leo nimefika mwisho, natumai hatua hii itawapatia wengine ujasiri wa kuacha yale ambayo yanawavuta nyuma. Nafanya juhudi kuwa bora na kuangalia watoto wangu, na kufanya biashara yangu. Hatua moja kwa wakati" Amesema Amira.

Haya yanajiri takriban miezi mitatu tu baada ya Amber Ray kuweka wazi kuwa ndoa yake na Jimal ilikuwa imepiga kikomo.

Akiwa katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram, Amber Ray alijibu shabiki aliyetaka kujua iwapo bado ako kwenye mahusiano na Jimal kuwa ako 'single'.