"Nilifutwa kazi nikisoma habari hewani!" mwanahabari afunguka

Muhtasari

• Moses Kanyiri - Amini usiamini, nilifutwa kazi huku nikisoma habari za saa saba mchana,   nilipokea simu iliyoniarifu kwamba huduma zangu hazikuwa zinaitajika tena katika kituo hicho

Mwanahabari Moses mwana wa Kanyiri
Mwanahabari Moses mwana wa Kanyiri
Image: Facebook

Mwanahabari maarufu wa lugha ya Kikuyu, Moses Kanyira aelezea kwa masikitiko makubwa jinsi ambavyo alifutwa kazi huku akiendelea kusoma habari za saa saba mchana katika kituo kimoja nchini ambapo alikuwa anafanya kazi.

Kanyiri katika ujumbe mrefu ambao aliuachia wikendi iliyopita kwa lugha ya Kikuyu kupitia ukurasa wake wa Facebook alieleza kwamba baada ya kufanya kazi kituoni hapo kwa miaka 17, fadhila aliyolipwa ni kufutwa kimadharau akiwa katikati ya kusoma habari za saa saba.

“Amini usiamini, nilifutwa kazi huku nikisoma habari za saa saba mchana. Wakati niliingia katika kipengele cha habari za kimataifa, nilipokea simu iliyoniarifu kwamba huduma zangu hazikuwa zinaitajika tena katika kituo hicho,” alifunguka Kanyiri kwa ujumbe mrefu ulioelezea matukio kwa lugha ya Kikuyu.

Alisema baada ya simu hiyo, hajui nini kilitokea lakini anakumbuka tu kupata nguvu na ujasiri wa kumalizia habari ambapo aliwataka kwaheri wasikilizaji na wafuasi wake na kuondoka.

Mwanahabari huyo alisema baada ya kuona kiza kinene, hatimaye Mungu alifungulia njia ambapo alipata tena kazi katika kituo kimoja cha runinga kinachopeperusha habari kwa lugha ya Kikuyu, akaajiliwa ambapo alifanya kazi kwa muda mfupi na kung’atuka.

Kwqa sasa, Kanyiri anaendeleza gurudumu la maisha kupitia kwa biashara yake aliyoianzisha baada ya kuachia ngazi katika kituo hicho cha runinga.