Zari Hassan ajibu madai ya kutoelewana na familia ya Diamond

Muhtasari

•Zariamesema amekosa kuwaelewa  baadhi ya Watanzania kwa sababu akitembelea familia hiyo au akose bado huwa wanamkosoa.

•Zari ameweka wazi kwamba uhusiano wake na familia ya Diamond ni mzuri na kusema hata huwa anawatembelea.

Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Mwanasoshalaiti Zari Hassan amelazimika kujitokeza kuwajibu wakosoaji wanaodai kuwa hana uhusiano mzuri na Mama Dangote.

Tetesi kuwa Zari hana maelewano mazuri na mama ya aliyekuwa mpenzi wake Diamond Platnumz zilichimbuka baada yake kuonekana jijini Dar Es Salaam ambako alikuwa ameenda kuhudhuria uzunduzi wa video ya msanii Juma Jux.

Baadhi ya wanamitandao walimsuta mzaliwa huyo wa Uganda wakidai kwamba alifika Dar na kudinda kumtembelea mamake Diamond ambaye ni baba ya watoto wake wawili. 

Zari aliwajibu wakosoaji wake huku akiweka wazi kwamba huwa anatembelea familia ya kina Diamond bila kutangaza. Alisema amekosa kuwaelewa  baadhi ya Watanzania kwa sababu akitembelea familia hiyo au akose bado huwa wanamkosoa.

"Nisipoenda Madale ama Mbezi wanasema ooh hawamtaki, hawajaonana naye. Nikienda wanasema Zari anapenda sana kukwamilia sana kwa hiyo familia. Nikienda mnaongea, nikikosa mnaongea! Hao watu huwa naongea nao. Mpaka nimefika pale nikawaambia hivi na hivi kikazini wakasema Sawa Mama T wewe furahia," Alisema

Mama huyo wa watoto watano alisema wanaomkosoa hawana cha kufaidi nacho wakati  akimtembelea Mama Dangote ama akose. Pia alisema sio sharti apakie picha mitandaoni kuthibitisha kuwa ameonana na mama mkwe huyo wake.

"Wengine wetu hatuishi maisha ya Instagram. Inaweza kuonekana hivyo lakini sio hivyo. Poleni mmekatishwa tamaa lakini ndiyo hivo," Alisema Zari.

Zari aliondoka nchini Tanzania mwaka wa 2018 baada ya kutengana na baba ya watoto wake Tiffah Dangote na Prince Nillan, Diamond Platnumz.

Baadae mwanasoshalaiti huyo alielekea Afrika Kusini ambako amekuwa akiishi huku akisimamia biashara zake kadhaa.

Zari na Diamond hata hivyo wamekuwa wakionana mara kwa mara na kushirikiana vizuri katika malezi ya watoto wao.