Harmonize afunguka somo muhimu alilopata kutoka kwa marehemu Steven Kanumba

Kanumba alifariki Aprili 7, 2012 kutokana na jeraha la kichwa alilopata baada ya kuanguka katika chumba chake cha kulala.

Muhtasari

•Harmonize amekiri kuwa alipata mafunzo mengi ya kimaisha kutoka kwa filamu za muigizaji huyo aliyeshabikiwa sana akiwa hai na hata baada ya kifo chake.

•Bosi huyo wa Konde Music Worldwide alimtakia Kanumba mapumziko ya amani huku miaka 10 ikiwa imepita tayari tangu kuaga kwake.

Harmonize, marehemu Steven Kanumba
Image: HISANI

Staa wa Bongo Harmonize amemsherehekea muigizaji wa filamu za Bongo, marehemu Steven Charles Kanumba.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmonize amekiri kuwa alipata mafunzo mengi ya kimaisha kutoka kwa filamu za muigizaji huyo aliyeshabikiwa sana akiwa hai na hata baada ya kifo chake.

Konde Boy alisema ingawa hakupata nafasi ya kukutana na marehemu, alijifunza unyenyekevu kwa kumtazama kwenye runinga.

"Kanumba made me to be so humble ingawa sijawahi hata kumuona mpaka anatangulia kifupi hanijuwi," Harmonize aliandika.

Bosi huyo wa Konde Music Worldwide alimtakia Kanumba mapumziko ya amani huku miaka 10 ikiwa imepita tayari tangu kuaga kwake.

Muigizaji huyo alifariki mnamo Aprili 7, 2012 kutokana na jeraha la kichwa baada ya kuanguka katika chumba chake cha kulala.

Wakati wa kifo chake, Kanumba alikuwa pamoja na aliyekuwa mpenziwe na pia muigizaji mwenzake, Bi Elizabeth Michael ambaye baadae alishtumiwa kwa mauaji yake na kushtakiwa kwa jaribio la mauaji.

Takriban miezi mitano iliyopita mamake Kanumba,  Bi Flora Mutegoa alitoa shukrani kubwa kwa bosi wa WCB, Diamond Platnumz kwa kumkumbuka marehemu mwanawe kwenye wimbo wake  'nawaza'.

Mjane huyo alisema aliridhishwa na kitendo cha  Diamond kumsherehekea mwanawe hasa katika kipindi hicho kilichokuwa cha kumbukumbu ya kifo chake.

"Ameweza kumkumbuka marehemu Steven Charles Kanumba. Haikuwa rahisi. Nilipousikia nilifarijika, nilifurahi sana, kumbe bado anamkumbuka! Mwezi ujao, tarehe saba tunamaliza  miaka kumi," Bi Mutegoa alisema akihutubia waandishi wa habari.

Mutegoa alisema ni jambo la maana kuona Diamond akimuwaza mwanawe kwani ni wengi ambao tayari wamemsahau mwigizaji huyo aliyeshabikiwa kote duniani.

Katika wimbo wake 'Nawaza', Diamond alisema  "Huenda Kanumba angelikuwepo hai, Nawaza movie zetu pia tungejidai."

Kila mwaka, muigizaji Wema Sepetu ambaye pia aliwahi kuwa kwenye mahusiano na Kanumba huwa anaadhimisha kifo chake.