Ringtone ajitolea kumwajiri Eric Omondi kama mjakazi ili kumtimiza tamaa ya kuishi Runda

Alisema yupo tayari kumpatia mchekeshaji huyo mshahara wa Ksh 50,000 kila mwezi.

Muhtasari

•Mwenyekiti huyo wa Muungano wa Wasanii wa Injili wa kujibandika alidokeza kuwa Bw Omondi amelemewa kabisa  na usanii.

•Ringtone alibainisha kuwa mchekeshaji huyo  hawezi  kumudu kuishi katika mtaa wa Runda kama yeye.

Ringtone Apoko na Eric Omondi
Image: INSTAGRAM//

Mwimbaji wa nyimbo za injili Alex Apoko almaarufu Ringtone amejitolea kumuajiri mchekeshaji Eric Omondi nyumbani kwake Runda, Nairobi.

Katika mahojiano na NTV, Ringtone alidai kuwa hatua hiyo yake itafanikisha ndoto ya Eric Omondi ya kuishi katika mtaa wa kitajiri wa Runda.

Mwenyekiti huyo wa Muungano wa Wasanii wa Injili wa kujibandika alidokeza kuwa Bw Omondi amelemewa kabisa  na usanii.

"Siku ingine nilimwambia akuje kwangu Runda nimuajiri kazi akakataa. Naweza kumwandika awe msimamizi wa kiwanja, hakuna kitu ingine. Eric Omondi hata talanta, labda naweza kumwandika kama kijakazi," alisema.

Ringtone alibainisha kuwa mchekeshaji huyo mwenye umri wa miaka 40 hawezi  kumudu kuishi katika mtaa wa Runda kama yeye.

Alisema iwapo Bw Omondi atakubali ofa yake basi yupo tayari kumpatia mshahara wa Ksh 50,000 kila mwezi.

"Anatamani maisha mazuri.Akuje nimpatie kazi ya mjakazi. Bila hivyo hawezi kuishi Runda. Naweza kumlipa 50,000. Hiyo ni pesa kidogo sana," alisema kabla ya kuonyesha noti za elfu moja alizokuwa nazo mfukoni.

Mwimbaji huyo alidai kuwa jumla ya pesa ambazo alikuwa amebeba katika studio za NTV ni shilingi laki moja.

"Ofa ya nafasi ya kazi ya unyenyekevu sana kwa kaka yangu Eric Omondi," alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Ugomvi na kudhalilishana kati ya Ringtone na Eric  hazijaanza leo wala jana, wawili hao wamekuwa wakikoseana heshima hadharani kwa muda.

Mwaka jana wakati mwimbaji huyo alipokuwa akizungumza na wanahabari katika sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Diana Marua,  alidai kuwa Eric Omondi ndiye mchekeshaji fukara zaidi nchini.

Ringtone  alidai kwamba Omondi ni ombaomba huku akimshtumu kutumia jina la wanamuziki kujenga taaluma yake.

"Eric Omondi hafai kukaa katika meza ya wasanii. Anaweza kuwa tu mcheza densi wetu. Yeye pamoja na waachekeshaji wengine ambao wanajaribu kuwa kama sisi ni wacheza densi. Wengi wamekuwa wakitoa vichekesho juu yetu ndio wajulikane.  Eric Omondi ako na wafuasi lakini hana pesa. Butita anashinda Eric Omondi. Mammito anashinda Eric Omondi.  Yeye ndiye maskini kabisa. Ukiangalia ameendesa gari moja kwa miaka 15. Hana pesa za kununua gari nyingine. Mimi naendesha gari kubwa. Eric Omondi anaendesha gari mzee inazima kila siku.Yeye lazima aombe. Jimi Wanjigi alimsaidia gari.  Sisi wasanii tunafanya kazi, tunanunua magari yetu hatusbiri kupewa zawadi" Apoko alisema.

Hapo awali Omondi alikuwa amedai kuwa mwimbaji huyo alifukuzwa katika nyumba yake ya Runda kwa kushindwa kulipa kodi, madai ambayo Ringtone alikana.Eric alidai kuwa Apoko alilazimika kuhamia eneo moja kando ya barabara ya Jogoo Road baada ya kufurushwa kutoka kwa jumba lake la Runda.