Harmonize amfariji Davido baada ya mwanawe kudaiwa kufariki

Ifeanyi anaripotiwa kufariki Jumatatu usiku baada ya kuzama kwenye kidimbwi cha kuogelea.

Muhtasari

•Ifeanyi ambaye hivi majuzi alitimiza umri wa miaka mitatu alikuwa akiogelea kwenye kidimbwi kilicho nyumbani kwao alipokufa maji.

•Harmonize ambaye ni rafiki wa karibu wa Davido amemtia moyo na kumhimiza awe na nguvu katika kipindi hiki kigumu.

Msanii DAVIDO
Msanii DAVIDO
Image: INSTAGRAM// DAVIDO

Staa wa Bongo Harmonize amemfariji mwimbaji mwenzake Davido kutoka Nigeria kufuatiana madai ya kifo cha mwanawe.

Mtoto wa Davido na mpenziwe Chioma, Ifeanyi anaripotiwa kufariki Jumatatu usiku baada ya kuzama kwenye kidimbwi cha kuogelea.

Kulingana na ripoti, Ifeanyi ambaye hivi majuzi alitimiza umri wa miaka mitatu alikuwa akiogelea kwenye kidimbwi kilicho nyumbani kwao katika eneo la Kisiwa cha Banana, Jimbo la Lagos, Nigeria alipokufa maji.

Inaripotiwa kwamba mvulana huyo mdogo alikaa chini ya maji kwa muda mrefu kabla ya hatimaye kuonekana na kukimbizwa katika hospitali ya Lagoon iliyo eneo la Ikoyi ambako alithibitishwa kufariki.

Davido na mpenziwe Chioma walikuwa wamesafiri hadi Ibadan kwa mkutano wa familia na walikuwa wamemwacha Ifeanyi na walezi wake ambao hawajaweza kueleza jinsi alivyoingia kwenye bwawa hilo bila kutambuliwa na hatimaye kuzama.

Maelfu ya wanamitandao wakiwemo watu mashuhuri tayari wamechukua hatua ya kumfariji mwimbaji huyo hata kabla ya yeye na mpenziwe kuthibitisha habari kuhusu kifo cha mtoto huyo wao.

Harmonize ambaye ni rafiki wa karibu wa Davido amemtia moyo na kumhimiza awe na nguvu katika kipindi hiki kigumu.

"Kuwa na nguvu kaka," aliandika chini ya picha ya mwimbaji huyo wa Afrobeats ambayo alipakia kwenye Instagram.

Wiki moja iliyopita, Davido aliandika ujumbe wa kipekee kwa mtoto wake mnamo siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwake. 

Aliandika:

"Ninaomba kwa moyo wangu wote kwamba Mungu akupe afya kamili na furaha safi kwa muda mrefu iwezekanavyo kibinadamu. Utakua na kuwa mkuu kuliko Mimi, Happy birthday mwanangu."