Watu 8 wafikishwa katika kituo cha polisi kufuatia kifo cha mwanawe Davido

Polisi wa Lagos wamethibitisha kifo cha mtoto wa Davido, Ifeanyi Adeleke.

Muhtasari

•Msemaji wa polisi wa Lagos alisema kwamba baada ya tukio hilo watu nane walifikishwa kituoni  kwa ajili ya mahojiano. 

• "Yeyote atakayepatikana na hatia ya kifo cha mtoto huyo atakamatwa" polisi alisema.

Msanii DAVIDO
Msanii DAVIDO
Image: INSTAGRAM// DAVIDO

Polisi katika Jimbo la Lagos nchini Nigeria wamethibitisha kifo cha mtoto wa Davido, Ifeanyi Adeleke.

Msemaji wa polisi wa Jimbo hilo Benjamin Hundeyin aliambia BBC kwamba baada ya tukio hilo watu nane walifikishwa kituoni  kwa ajili ya mahojiano. 

"Watu wanane waliletwa kwa mahojiano na baada ya uchunguzi wa kina, yeyote atakayepatikana na hatia ya kifo cha mtoto huyo atakamatwa" alisema.

Mtoto wa Davido na mpenziwe Chioma Rowland, Ifeanyi anaripotiwa kufariki Jumatatu usiku baada ya kuzama kwenye kidimbwi cha kuogelea.

Kulingana na ripoti, Ifeanyi ambaye hivi majuzi alitimiza umri wa miaka mitatu alikuwa akiogelea kwenye kidimbwi kilicho nyumbani kwao katika eneo la Kisiwa cha Banana, Jimbo la Lagos, Nigeria alipokufa maji.

Inaripotiwa kwamba mvulana huyo mdogo alikaa chini ya maji kwa muda mrefu kabla ya hatimaye kuonekana na kukimbizwa katika hospitali ya Lagoon iliyo eneo la Ikoyi ambako alithibitishwa kufariki.

Davido na mpenziwe Chioma walikuwa wamesafiri hadi Ibadan kwa mkutano wa familia na walikuwa wamemwacha Ifeanyi na walezi wake ambao hawajaweza kueleza jinsi alivyoingia kwenye bwawa hilo bila kutambuliwa na hatimaye kuzama.

Maelfu ya wanamitandao wakiwemo watu mashuhuri tayari wamechukua hatua ya kumfariji mwimbaji huyo hata kabla ya yeye na mpenziwe kuthibitisha habari kuhusu kifo cha mtoto huyo wao.

Wiki moja iliyopita, Davido aliandika ujumbe wa kipekee kwa mtoto wake mnamo siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwake. 

Aliandika:

"Ninaomba kwa moyo wangu wote kwamba Mungu akupe afya kamili na furaha safi kwa muda mrefu iwezekanavyo kibinadamu. Utakua na kuwa mkuu kuliko Mimi, Happy birthday mwanangu."