Staa wa reggea Ce'cile amsherehekea 'mumewe' Mkenya

Mike alimtambua mwanamuziki huyo mahiri kama mpenzi wake

Muhtasari

•Katika ujumbe wake wa kheri ya siku ya kuzaliwa, Ce'cile alimtambulisha Bw Mike kama mume wake kutoka Kenya.

•"Asante mpenzi, acha nikutumie maelezo sasa hivi," Mike alijibu.

Image: TWITTER// CE'CILE

Siku ya Jumanne, mwimbaji maarufu wa reggea kutoka Jamaica Cécile Claudine Charlton alimsherehekea mfanyibiashara mmoja wa Kenya.

Mfanyibiashara Mike Gichohi alikuwa akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa na Ce'cile ambaye ni miongoni mwa wasanii wa reggea wanaoshabikiwa sana nchini Kenya alikuwa mmoja wa waliomsherehekea kwa ujumbe wa kheri njema.

Katika ujumbe wake wa kheri ya siku ya kuzaliwa, Ce'cile alimtambulisha Bw Mike kama mume wake kutoka Kenya.

"Kheri ya siku ya kuzaliwa mume wangu Mkenya.. mtandao wako wa pesa ni upi," alimwandikia kupitia mtandao wa Twitter.

Malkia huyo wa reggea aliambatanisha ujumbe wake na picha ya Mike.

Katika jibu lake kwa Ce'cile, Mike ambaye alikuwa akisherehekea kutimiza miaka 34 alimtambua mwanamuziki huyo mahiri kama mpenzi wake na kumshukuru kwa ujumbe wake mtamu wa siku ya kuzaliwa.

"Asante mpenzi, acha nikutumie maelezo sasa hivi," alijibu.

Imeweza kubainika kuwa sio mara ya kwanza kwa Ce'cile kumsherehekea mfanyibiashara huyo mnamo siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwake.

Mwaka jana, mwimbaji huyo alimtambua Mike kama mfalme wake na kuahidi kumletea zaidi katika ziara yake nyingine ya Kenya.

"Mike wangu. Kheri ya siku ya kuzaliwa mfame wangu wa Kenya. Numero uno @Mike4rmRuaiKE uwe na siku yenye baraka. Tuonane hivi karibuni. Nitaleta zawadi yako," alimwambia.

Ce'cile ni miongoni mwa wasanii wa Jamaica wanaopenda kutembea na kutumbuiza hapa nchini Kenya.  Alifanya ziara ya Kenya mara ya mwisho takriban miaka mitano iliyopita.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 48 aliwahi kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwimbaji wa reggea mwenzake Christopher Martin.  Wawili hao ambao walichumbiana kwa takriban miaka minne wako na mtoto mmoja pamoja.