Kusherehekea Krismasi ni utoto! - Pastor Ezekiel awaambia waumini (Video)

mchungaji huyo alisema sherehe hizo ni za watoto na watu wazima hawafai kusherehekea.

Muhtasari

• Aliwataka watu kuwachinjia watoto kuku na kuwaacha washerehekee lakini wao wenyewe wajilishe chakula cha kiroho.

• Aliwataka kujiuliza kama wamewahi ona faida yoyote ya kusherehekea Krismasi tangu wazaliwe.

Mchungaji Ezekiel Odero amewasuta na kuwashtumu vikali waumini wa Kikristo wanaosherehekea Krismasi kwa kuchinja na kula kuku.

Kulingana na mchungaji huyo, kusherehekea Krismasi ni utoto ambao unafaa kuachwa na waumini ambao wanafuata tamaduni hiyo kuwa ni siku Yesu alizaliwa.

Odero alisema kuwa kusherehekea Krismasi kunafaa kuachiwa watoto wadogo lakini kwa watu wazima kujikita katika kusherehekea Krismasi ni utoto mkubwa ambao hauna tija yoyote.

Odero aliwauliza waumini katika kanisa lake ni kwa nini huwa wanang’ang’ana kufuga kuku ili siku ya Desemba 25 wamchinja akisema kuwa huo ni utoto mwingi.

“Mimi nakuuuliza swali moja tu mtu wa Mungu, leo umefunga kuku, kwani wewe ni mtoto? Ni mara yako ya kwanza mpaka uchinje kuku siku ya Krismasi? Si utulie tu ulishe watoto lakini mwenyewe ujilishe chakula cha kiroho. Kuwa mtu mzima. Wakati ule unang’ang’ana kusherehekea Krismasi wenzako wanaendelea kufanya kazi. Hebu jaribu kujiuliza ni mara ngapi umekuwa ukisherehekea Krismasi na mabadiliko yapi umewahi pata maishani mwako,” mchungaji huyo alisema.

Mchungaji huyo mwenye utata amekuwa akihubiri kuhusu masuala ya utata na kuwakanya waumini wake dhidi ya kufanya mambo kama hayo.

Mwaka jana, Odero aligonga vichwa vya habari ndani na nje ya Kenya baada ya kujaza dimba la Kasarani jijini Nairobi kwa waumini wake wengi katika kongamano la kiroho.

Mchungaji huyo pia amewahi nukuliwa akiwaonya waumini wake haswa jamii za Luhya na Waluo dhidi ya kusherehekea katika mazishi na kununua majeneza ghali katika kile alikitaja kuwa kufanya hivyo ni kufurahisha roho ya umauti ili irudi tena kugharimu maisha ya mwanafamilia mwengine.