Wanaume wanahitaji mwanamke mwenye 'uDelilah' fulani kwenye ndoa - Mchungaji ashauri

Ulokole na unyenyekevu ni kanisani, tukifika nyumbani sisi ni viumbe tofauti," mchungaji huyo wa kike alishauri wanawake.

Muhtasari

• Mchungaji huyo alisema kwamab ushauri wake si wa kubomoa ndoa bali ni kwa manufaa ya ndoa imara.

• Alisema kwamba ndoa nzuri hutoa watoto wazuri wenye kumcha Mungu.

Mchungaji wa kike ashauri wanawake kuchukua uDelilah katika ndoa.
Mchungaji wa kike ashauri wanawake kuchukua uDelilah katika ndoa.
Image: Instagram

Mchungaji wa kike maarufu kutoka Tanzania Rose Shaboka amewashauri wanawake katika ndoa kuiga baadhi ya tabia kama za mwanamke Delilah katika Biblia ili kudumisha ndoa zao.

Kulingana na mchungqaji Shaboka, ili kuimudu ndoa yako wewe kama mwanamke, ni sharti uweke kile ambacho alikiita ‘uDelilah’ kiasi katika ndoa hiyo ili kuisimamisha kwa nguzo imara.

“Hawa viumbe wanataka mwanamke Fulani mwenye uDelilah. Wanataka mwanamke ambaye akili yake ina uDelilah. Unajitoa ufahamu,” mchungaji huyo alishauri kundi la wanawake darasani huku wakimshangilia.

Alisema kwamba wanawake wanafaa kuleta na kuonesha ulokole wakiwa kanisani kunyenyekea mbele ya Mungu lakini wakirudi nyumbani wanafaa kukaza nati kidogo kwa waume zao, kwa manufaa ya ndoa zao.

“Hapa ndio tunaleta ulokole, tukifika kule nyumbani sisi ni viumbe tofauti. Sisi ni viumbe wengine, wa kuwapa raha hawa wajamaa.”

“Sasa wewe Mara zote umenuna, nywele zenyewe mwezi ukisuka huendi kuziosha mpaka zinatoa harufu. Watu wa Mungu tunamuitaji ili kuboresha hizi ndoa. Shetani anazishambulia kwa sababu anajua kilichopo. Ndoa ikikaa sawa ndio inatoa watoto wa maana,” alishauri.

Kutoka kitabu cha Biblia, mwanamke Delilah anaelezewa kuwa mwanamke mmoja ambaye alitumiwa na jamii hasimu ya Wafilisti ili kuifichua siri ya nguvu za ajabu ambazo zilikuwa zinamilikiwa na hakimu wa kwanza wa Waisrael, Samson.

Delilah anaelezewa kwamba alijijongeza kwa Samson kwa njia ya kimapenzi lakini lengo na nia yake kuu ilikuwa ni kupata siri ya nguvu zake ambazo zilikuwa za kuwashangaza Wafilistina, ikiwemo kuangusha kuta imara, kuua simba kwa mikono yake miongoni mwa mambo mengine makubwa.

Alipofika kwa Samson, alimtaka kumpa siri ya nguvu zake kama kweli anampenda, na kwa kupumbazwa na mapenzi, maskini Samson alifichua siri ya nguvu zake kuwa ilikuwa kwa nywele, Delilah alinyata nje na kufichua siri hiyo kwa Wafilisti ambao walimnyoa Samson na hivyo kulemaza nguvu zake.