Watoto wa marehemu mchungaji T.B Joshua waibuka kufanya miujiza Tanzania

Wawili hao waliita huduma yao kama kliniki ya uponyaji na kusema wako tayari kuwapokea wagonjwa kwa ajili ya maombi ya kuwapa uponyaji kabisa.

Muhtasari

• Wawili hao walijitaja kuwa mfanano wa Petro na Yohana kwenye Biblia ambao walimponya kiwete aliyekuwa ameketi kwenye lango la kuingia kwenye synagogue.

• Vijana hao wawili, mmoja akiwa kutoka taifa la Tanzania na mwingine kutoka Ethiopia walitangaza mkusanyiko mkubwa wa uponyaji nchini Tanzania

Watoto wa mchungaji TB Joshua waibuka na ibada ya uponyaji Tanzania.
Watoto wa mchungaji TB Joshua waibuka na ibada ya uponyaji Tanzania.
Image: Screengrab//YouTube

Wanaume wawili wanaodai kuwa watoto wa kiroho wa kanisa la mchungaji aliyefariki miaka miwili iliyopita kutoka nchini Nigeria, T.B Joshua wameibuka na kudai kwamba watashusha miujiza ya kushangaza katika taifa jirani la Tanzania.

Vijana hao wawili, mmoja akiwa kutoka taifa la Tanzania na mwingine kutoka Ethiopia walitangaza mkusanyiko mkubwa wa uponyaji nchini Tanzania ambalo limeanza Ijumaa na kukamilika Jumapili na baadae Jumatatu wiki kesho kuwa na mkutano wa wanandoa.

“Nataka kumkaribisha nabii ambaye ni ndugu yangu katika Kristo. Wote tumekuwa katika huduma kama watoto wa marehemu nabii T.B Joshua kwa muda mrefu, kwa hiyo ni kaka yangu katika Yesu,” mtoto huyo wa Joshua kutoka Tanzania alimkaribisha mwenzake kutoka Ethiopia.

Wawili hao walisema wameleta huduma maalum ya uponyaji nchini Tanzania ambayo itashuhudia miujiza ya kuwaokoa watu kutoka mateso, kuwaponya na kadhalika.

“Hii program inaanza Ijumaa na tumeiita kliniki ya uponyaji. Kuanzia asubuhi tutawapokea wagonjwa na kuwafanyia screening na baadae nabii atafika na tutaanza kuhudumia,” alisema.

Wawili hao walijitaja kuwa mfanano wa Petro na Yohana kwenye Biblia ambao walimponya kiwete aliyekuwa ameketi kwenye lango la kuingia kwenye synagogue.

Mchungaji T.B Joshua muasisi wa kanisa la Synagogue Church of All Nations alifariki mwaka 2021 akiwa na umri wa miaka 57 na vyombo vingi vya habari vilimtaja kama mchungaji aliyekuwa na skendo nyingi haswa katika mafunzo yake kwa waumini wa kanisa hilo lake jijini Lagos, Nigeria.

Baba huyo wa watoto watatu alikuwa mmoja wa wahubiri wenye ushawishi mkubwa barani Afrika na mamilioni ya wafuasi wa televisheni na mitandao ya kijamii. Zaidi ya watu 15,000 kutoka Nigeria na nje ya nchi walikuwa wanahudhuria ibada zake za Jumapili.

"Mungu amemchukua mtumishi wake Nabii TB Joshua nyumbani ... dakika zake za mwisho duniani alizitumia katika kumtumikia Mungu," kanisa liliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kipindi hicho, bila kutoa maelezo zaidi.