Pritty Vishy atupa vijembe baada ya mke wa Stivo Simple Boy kufichua masaibu ya msanii huyo

Vishy aliikosoa ndoa a ya sasa ya mwimbaji huyo kutoka Kibra akiashiria kuwa yeye ndiye alikuwa mshirika bora kwake.

Muhtasari

•Pritty Vishy alibainisha kuwa watu walidhani kwamba bado alikuwa amekwama kwake baada ya kujaribu kufichua tishio hilo.

•Grace alibainisha kuwa licha ya kuwa na jina kubwa, mumewe anakabiliwa na changamoto za kifedha kwani havuni chochote kutokana na muziki wake.

Stivo Simple Boy na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy
Stivo Simple Boy na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy
Image: SCREENGRAB// MUNGAI EVE

Mpenzi wa zamani wa mwimbaji Stivo Simple Boy, Pritty Vishy amewakumbusha Wakenya kuwa aliahi kufichua matatizo mwimbaji huyo anakabiliana nayo lakini hakuna aliyemwamini.

Huku akitoa maoni baada ya mke wa sasa wa rapa huyo, Grace Atieno kufunguka kuhusu matatizo ya kifedha na usimamizi ambayo mwimbaji huyo anakabiliana nayo, Vishy alibainisha kuwa watu walidhani kwamba bado alikuwa amekwama kwake baada ya kujaribu kufichua tishio hilo.

Wakati huo huo, alionekana kuirushia vijembe ndoa ya sasa ya mwimbaji huyo kutoka Kibra akiashiria kuwa yeye ndiye alikuwa mshirika bora kwake.

“Nilisema lakini wote mlisema sijasonga mbele na maisha yangu. Sasa tuone. Somo lililopo ukiwa na mwanamke sahihi kando yako, mthamini kila mara na uwe na shukrani,” Pritty Vishy alisema kwenye Instagram.

Hii ilikuwa baada ya mkewe Stivo, Bi Grace Atieno kufunguka kuhusu masaibu ambayo yeye na msanii huyo wanapitia nyumbani.

Katika mahojiano na Vincent Mboya, mrembo huyo kutoka Taita Taveta alibainisha kuwa licha ya kuwa na jina kubwa, mumewe anakabiliwa na changamoto za kifedha kwani havuni chochote kutokana na muziki wake.

Grace alimshtumu meneja wa Stivo kwa kumhujumu na kujinufaisha na jasho lake.

“Stivo anapitia maisha magumu. Yeye ni mtu muoga na kijana mpole. Kuna mambo anapitia lakini ni muoga wa kuongea. Kuna marafiki wake na mashabiki hutamani kuchat na yeye lakini hawawezi kumkuta,” Grace alilalamika.

Aliongeza, “Najua watu wengi wanajua Stivo ni yeye hutumia Tiktok yake na Instagram, lakini sio yeye. Wengi huwa wanalalamika kwamba wanataka kumsaidia na kitu kidogo lakini hawamkuti. Yaani anapitia changamoto nyingi tu.. Hana akaunti yoyote anayotumia. Meneja wake ako na kila kitu chake. Hata kumpata, huwezi kumkuta kwa urahisi.”

Bi Grace alifichua kwamba mumewe ata hafahamu  kiasi cha pesa ambacho huwa analipwa kwa kila shoo. Alisema meneja wake ndiye anayendeleza na kusimamia kila kitu ikiwemo akaunti zote za mitandao ya kijamii, mawasiliano na hata malipo.

Alibainisha kwamba matatizo ya kifedha nyumbani hufanya wanagombana mara kwa mara ila wanavumilia tu.

 “Tunapitia magumu ni ile tu huwezi kutoka nje kuomba mtu nini na nini, tunavumilia tu. Wakati mwingine tunagombana kutokana na hizo tu changamoto lakini ukimwambia aende aongee na meneja wake mambo ya hela ajisimamie mwenyewe anaogopa,” Grace alisema.

“Kuna saa zingine twapata, saa zingine tunakosa. Yeye hana kazi eti anaweza akasema atatoka huku nje afanye ili apate pesa atafute chakula. Ni hiyo tu kazi moja ambayo anategemea na hiyo kazi ambayo anategemea hamna chochote. Meneja wake ndiye amebeba pesa, amebeba kila kitu,” alilalamika.

Grace aliwaomba watu walio na nia ya kumsaidia mtunzi huyo wa kibao ‘Mihadarati’ kumfikia moja kwa moja badala ya kumtumia meneja huyo.