Mrembo wa Ethiopia, Nabayet aweka mambo wazi kuhusu kuwa na mimba ya Otile Brown

Baadhi ya wanamitandao walimpongeza mrembo huyo kwa 'ujauzito’ na kumtakia kujifungua salama.

Muhtasari

•Mpenzi wa zamani wa Otile Brown, Nabayet almaarufu Nabbi amedokeza kuwa sio yeye mzazi mwenza mtarajiwa wa mwimbaji huyo.

•Huku akijibu uvumi huo, mlimbwende huyo aliweka wazi kuwa hana ufahamu kuwa ni mjamzito lakini akawashukuru mashabiki kwa utani.

Otile Brown na Nabayet katika picha ya maktaba.
Image: HISANI

Aliyekuwa mpenzi wa Otile Brown, Nabayet almaarufu Nabbi amedokeza kuwa sio yeye mzazi mwenza mtarajiwa wa mwimbaji huyo.

Baada ya staa huyo wa muziki wa Kenya kutangaza kwamba atakuja kuwa mzazi hivi karibuni siku ya Jumamosi, baadhi ya mashabiki walikisia kuwa mwanamke aliyekuwa akitarajia mtoto naye si mwingine bali ni mwanadada huyo mrembo kutoka Ethiopia ambaye alichumbiana naye kwa miaka kadhaa.

Baadhi ya wafuasi wa Nabbi kwenye mitandao ya kijamii walimpongeza kwa ‘ujauzito’ huo na kumtakia kujifungua salama.

"Nina furaha sana wanandoa ninaowapenda sana wanapata mtoto," shabiki mmoja alimwandikia kwenye mtandao wa Instagram.

Shabiki mwingine alimwambia, "Tunajua wewe ni mjamzito, hongera."

Huku akijibu uvumi huo, mlimbwende huyo aliweka wazi kuwa hana ufahamu kuwa ni mjamzito lakini akawashukuru mashabiki kwa utani.

"Lol, sikujua lakini asante," Nabbi aliandika na kuambatanisha na emoji za kicheko kuashiria madai hayo ni uvumi tu.

Huku akitangaza anatarajia mtoto wake wa kwanza siku ya Jumamosi jioni, mwimbaji Otile Brown ambaye kwa jina halisi ni Jacob Obunga aliahidi kumpa mtoto atakayezaliwa upendo wake wote.

"Bizeee hivi karibuni atakuwa papa, Inshallah.. Nitakupenda sana mtoto #Inshaallah," Otile Brown alisema kupitia mtandao wa Instagram.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 30 hata hivyo hakufichua maelezo ya mzazi mwenzake au jinsia ya mtoto anayetarajia.

Tangu kutangaza utengano wake na mrembo wa Ethiopia, Nabayet mapema mwaka jana, Otile Brown amekuwa msiri  sana kuhusu mahusiano yake.

Mwimbaji Otile Brown alithibitisha kutengana kwake na Nabbi mnamo wezi Januari mwaka jana baada ya kuchumbiana naye kwa karibu miaka mitatu. Wawili hao walijitosa kwenye mahusiano mapema mwaka wa 2019, miezi michache tu baada ya Otile kutengana na mwanasoshalaiti maarufu Vera Sidika.

Wakati akitangaza kutengana kwao kupitia ukurasa wake wa Instagram, Otile alifichua kuwa mara ya mwisho alipokutana na Nabbi alitaka kujua jinsi wangeendelea na wakakubaliana kwenda tofauti.

"Mimi na Nabbi hatuko pamoja tena… Mara ya mwisho tulikuwa pamoja ilikuwa kujaribu kutafuta njia ya kusonga mbele lakini tuliamua kwenda tofauti kwa bahati mbaya," Mwanamuziki huyo alisema.