Ex wako anaweza kukushtaki kwa kumuahidi ndoa - Mwanasheria anaeleza

"Kama mtu atakuambia atakuoa na baadae aseme hataki kuoana na wewe, hapo mkataba utakuwa umevunjwa na ndio maana tunasema ni kuvunja agano la ndoa,”

Muhtasari

• Wakili huyo hata hivyo alisisitiza kwamba ni lazima mtu aoneshe ushahidi mahakamani kwamba aliyekuwa mpenzi wake kweli alimuahidi ndoa.

Mume amuacha mkewe siku mbili baada ya kufunga harusi kisa alipigania chakula na mamake siku ya harusi.
Mume amuacha mkewe siku mbili baada ya kufunga harusi kisa alipigania chakula na mamake siku ya harusi.
Image: BBC NEWS

Wakili mmoja kutoka taifa la Ghana amezua gumzo mitandaoni baada ya kueleza kwamba kisheria, mtu unaweza kumshtaki aliyekuwa mpenzi wako iwapo alikuahidi ndoa lakini mwisho wa siku akabatili ahadi yake kwako.

Ernestina Obboh Botchwey alieleza kwamba kisheria pindi tu baada ya mtu kumposa mpenzi wake na huyo mpenzi kukubali, tayari hayo ni maagano tosha ambayo hayafai kukiukwa kwa namna yoyote ile.

Kubatili agano hilo ni sawa na kukiuka sehemu ya sheria na unaweza kashtakiwa na mpenzi huyo kwa kumhadaa.

Alisema kuwa wapenzi wenye huzuni wanaweza wakashtaki kwa kuharibiwa na hata kutaka kulipwa kwa uharibifu uliotokea kwako kwa ahadi za uongo kuhusu ndoa.

“Katika sheria, tunaona kwamba ahadi ya ndoa ni kama mkataba. Kama mtu atasema kwamba atakuoa na wewe useme nimekubali, basi hilo ni agano. Ni makubaliano kwamba mtu amekubali kuoana na wewe. Kwa hiyo kubadilishana kwa wawili hao kwa ahadi za ndoa ni tafsiri ya agano au mkataba. Kwa hiyo kama mtu atakuambia atakuoa na baadae aseme hataki kuoana na wewe, hapo mkataba utakuwa umevunjwa na ndio maana tunasema ni kuvunja agano la ndoa,” alinukuliwa.

Wakili huyo hata hivyo alisisitiza kwamba ni lazima mtu aoneshe ushahidi mahakamani kwamba aliyekuwa mpenzi wake kweli alimuahidi ndoa ili pia kumpa nafasi mshtakiwa kujitetea na sababu zake ni kwa nini alibatilisha ahadi ya kuoa au kuolewa na mwenzake.

Aliendelea kusema kwamba hata hivyo, mahakama haina mamlaka yoyote ya kushrutisha aliyekiuka ahadi ya kuoa au kuolewa kufanya hivyo kwani maamuzi yake yanajisimamia na kitakachotokea pengine akipatikana na hatia ni kutoa fidia tu kwa kumharibia muda na kumletea usumbufu mlalamikaji.

Baadhi ya watu walikubaliana na maelezo ya wakili huyo huku wengine wakisema kuwa itakuwa afueni haswa kwa watoto wa kiume ambao wanawaposa warembo na kukubali kuolewa nao lakini siku chache baadae warembo wale baada ya kuwafyonza akiba zao wanawaacha hoi bin taabani.