Korti yamtaka mke aliyemtaliki mume siku 11 baada ya kushinda 272m kumpa zote mumewe!

Siku 11 baada ya kushinda hela hizo, Denise Rossi alianzisha mchakato wa kumtaliki mumewe, Thomas Rossi na hivyo kuivunja ndoa yake iliyodumu kwa miaka 25.

Muhtasari

• Mipango yake yote ilionekana kuyumba baada ya kampuni hiyo ya bahati nasibu kuituma hundi ile kwa nyumba ya mumewe miaka miwili baadae, bila kujua kwamba wawili hao walitalikiana.

• Jaji wa mahakama ya familia ya Los Angeles alikubaliana na Thomas na kumpa pesa zote za bahati nasibu ya Denise.

Mwanamke atakiwa kumpa mumewe hela zote alizoshinda.
MAHAKAMANI: Mwanamke atakiwa kumpa mumewe hela zote alizoshinda.
Image: Maktaba,

Ni pigo kubwa kwa mwanamke mmoja nchini Marekani  baada ya mahakama kumuamrisha kumpa mumewe kila kitu baada ya kumtaliki.

Kwa mujibu wa nyaraka za mahakamani, mwanamke huyo, Denise Rossi alishinda jackpot katika mchezo wa bahati nasibu, ambapo alijinyakulia kitita cha shilingi milioni 272 za Kenya.

Siku 11 baada ya kushinda hela hizo, Denise Rossi alianzisha mchakato wa kumtaliki mumewe, Thomas Rossi na hivyo kuivunja ndoa yake iliyodumu kwa miaka 25.

Hata hivyo, hakumuambia mumewe kuhusu kushinda hela hizo wala katika hati ya mahakamani akitaka talaka, hakutaja kuwa alikuwa ameshinda hela bali alitaja sababu zake kuwa ni kuchoka tu na ndoa na alipania kuwa mtu huru asiyebanwa kwenye agano la ndoa.

Mipango yake yote ilionekana kuyumba baada ya kampuni hiyo ya bahati nasibu kuituma hundi ile kwa nyumba ya mumewe miaka miwili baadae, bila kujua kwamba wawili hao walitalikiana.

Thomas alipigwa na butwaa kujua kwamba mke wake wa zamani alikuwa ameshinda miluioni 272 katika Bahati Nasibu ya Jimbo la California na amekuwa akipokea shilingi milioni 4.5 kila mwaka.

Alimshtaki kwa kukiuka sheria za ufichuzi wa mali ya serikali na kutenda kwa ulaghai na kwa nia mbaya.

Jaji wa mahakama ya familia ya Los Angeles alikubaliana na Thomas na kumpa pesa zote za bahati nasibu ya Denise. Hakimu alisema kwamba Denise angeweza kuhifadhi nusu ya pesa hizo ikiwa angekuwa mwaminifu tangu mwanzo, lakini alipoteza haki yake ya kuzipata kwa kuzificha, jarida la mjini Los Angeles liliripoti.