Kajala afunguka kwa nini atahifadhi tattoo za Wema Sepetu na kufuta ya Harmonize

Muigizaji Kajala Masanja amedokeza kuwa anakusudia kufuta tattoo ya Harmonize kwenye kidole chake.

Muhtasari

•Kajala ameapa kuwa hatochorwa tattoo ya mtu mwingine yeyote katika maisha yake baada ya yaliyotokea kati yake na  Harmonize.

•Mama huyo wa binti mmoja alidokeza kwamba alichorwa tattoo hiyo wakati akiwa kwenye mapenzi mazito na Harmonize.

Harmonize, Kajala, Wema Sepetu
Image: HISANI

Muigizaji mkongwe wa filamu bongo, Fridah Kajala Masanja amedokeza kuwa anakusudia kufuta tattoo ya Harmonize kwenye kidole chake.

Katika kipande kidogo cha kipindi cha filamu yao ya uhalisia ya ‘Behind The Gram’ kitakachoonyeshwa siku ya Ijumaa, mama huyo wa binti mmoja alidokeza kwamba alichorwa tattoo hiyo wakati akiwa kwenye mapenzi mazito.

“Inabidi nifute tattoo hii. Nilifanya kwenye mapenzi. Ni mtu ambaye nilikuwa napenda,” Kajala alisema huku akionyesha herufi ‘R’ iliyochorwa kwenye kidole chake cha mkono wa kushoto.

‘R’ ni herufi ya kwanza ya jina halisi la Harmonize ambalo ni Rajab Abdul Kahali na ilichorwa kwenye kidole cha muigizaji huyo mwaka jana wakati mahusiano yao yalipokuwa yamechacha. Wawili hao hata hivyo waliachana mwishoni mwa mwaka jana na hawajawa na uhusiano mzuri tangu wakati huo.

Kajala sasa ameapa kuwa hatochorwa tattoo ya mtu mwingine yeyote katika maisha yake baada ya yaliyotokea kati yake na bosi huyo wa Konde Music Worldwide.

“Kwanza sitakuja katika maisha yangu tena kumchora mtu yaani kama mpenzi, mpenzi, ama nini,” Kajala alisema.

Mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize wakati huo huo alitangaza kwamba ataendelea kuhifadhi tattoo ya muigizaji mwenzake Wema Sepetu iliyochorwa mgongoni mwake.

Kajala alibainisha kuwa licha ya migogoro yao ya hapo awali, bado ana heshima kubwa kwa mpenzi huyo wa mwimbaji Whozu ambaye anaaminika kumtoa jela wakati alikuwa amefungwa miaka kadhaa iliyopita.

“Nina na tattoo nyingine ambayo ni ya umuhimu pia, ni tattoo ya Wema ambayo siwezi kuifuta kabisa. Tushapitia kwa ugomvi mwingi, sio zozo. Itakaa hapo kwa sababu ni mtu namheshimu nampenda,” alisema.

Mapema mwaka huu,Harmonize alichukua hatua ya kufuta tattoo kubwa ya mpenzi huyo wake wa zamani na binti yake Paula Paul ambayo alichorwa kwenye mguu wake mwaka jana.

Mwaka jana, wakati akiomba msamaha na kumsihi Kajala amrudie, Harmonize alipiga hatua ya kuchorwa tattoo ya picha ya kumbukumbu ya muigizaji huyo akiwa na bintiye Paula kwenye mguu wake. Alichukua hatua hiyo kama mojawapo ya njia ya kumtongoza ili warudiane baada ya kuwa wamekosana kwa mwaka.

Baadaye, wote wawili walichukua hatua ya kuchorwa herufi za kwanza za jina la kila mwingine wakati mahaba yalikuwa yamenoga.