"Mapenzi hutoka mbali!" Karen Nyamu asherehekea safari ndefu ya penzi lake na mwimbaji Samidoh

Wapenzi hao walikuwa wametembelea maporomoko ya Thompson katika eneo la Nyahururu, mwaka wa 2020.

Muhtasari

•Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu alionyesha kumbukumbu yake na mzazi mwenzake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh.

•Wapenzi hao mashuhuri walionekana kuwa na furaha pamoja na tabasamu kubwa ziliandikwa kwenye nyuso zao.

Samidoh na mpenzi wake Karen Nyamu
Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Siku ya Alhamisi, ikiwa TBT, seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu alionyesha kumbukumbu yake na mzazi mwenzake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh.

Kwenye ukurasa wake wa Facebook, seneta Karen Nyamu alichapisha picha iliyomuonyesha akiwa amemkumbatia mwimbaji huyo wa Mugithi kimahaba na kutumia fursa hiyo kusherehekea safari ya penzi lao.

Pichani, wawili hao walikuwa wametembelea maporomoko ya Thompson katika eneo la Nyahururu, mwaka wa 2020.

"Akorwo mwendwa wee no uririkane tusherete Nyahururu kirurumo-ini," Karen Nyamu aliandika kwa lugha ya Kikuyu.

Kumaanisha: "Kama wewe mpenzi unaweza kukumbuka tukiwa tumetembelea maporomoko ya maji huko Nyahururu.”

Aliongeza, "Mwaka wa TBT ni 2020! Wendo umaga kuraya. (Mapenzi hutoka mbali)

Katika picha hiyo, wapenzi hao mashuhuri walionekana kuwa na furaha pamoja na tabasamu kubwa ziliandikwa kwenye nyuso zao.

Mwanasheria huyo na mwimbaji wa Mugithi huyo wamekuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa miaka kadhaa na tayari wamejaliwa watoto wawili pamoja. Haijabainika ni lini hasa walianza kuchumbiana lakini mahusiano yao yalijulikana wazi hadharani mwaka wa 2021 kufuatia ripoti kwamba Samidoh ndiye baba mzazi wa mtoto wa pili wa seneta huyo, Sam Jr ambaye alizaliwa mwishoni mwa 2020.

Wiki za hivi majuzi, Nyamu amekuwa akitumia wakati mzuri na Samidoh katika wiki wakati mke wa mwimbaji huyo wa Mugithi akiaminika kuwa Marekani ambapo anafurahiya muda na watoto wake na marafiki wengine.

Wapenzi hao walimpokea mtoto wao wa pili, msichana mwaka jana na penzi lao limeonekana kuendelea kunoga kila uchao.

Hata hivyo, kwa muda mrefu kumekuwa na mzozo kati ya seneta Nyamu na mke wa kwanza wa mwimbaji huyo, Edday Nderitu.

Mwezi Februari, Bi Edday alimwandikia Samidoh ujumbe mrefu kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akimuonya kwamba hayuko tayari kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi. Hii ilikuwa baada ya msanii huyo kuonekana na mzazi mwenzake, Karen Nyamu licha ya awali kudaiwa uhusiano wao umefika mwisho.

Edday alimtaja Bi Nyamu kama mtu asiye na maadili na asiyeheshimu familia yake. Alidokeza kuwa takriban miaka mitatu iliyopita ya ndoa yake imejawa na maumivu na fedheha nyingi. Hata hivyo, alisema licha ya yote amebaki mwaminifu na ameendelea kuunga mkono kazi ya msanii huyo wa nyimbo za Kikuyu.