Vera adokeza kuwa na uhusiano mbaya na Huddah, afichua mara ya mwisho walipozungumza

Mwanasosholaiti huyo alifichua kuwa zaidi ya muongo mmoja umepita tangu alipozungumza na Huddah mara ya mwisho.

Muhtasari

•Vera Sidika amedokeza kuwa hana uhusiano wa karibu na mwanasosholaiti mwenzake Huddah Monroe.

•Mwaka wa Oktoba 2019, Vera alisema aliwahi kuwasiliana na Huddah Monroe kufanya biashara, lakini juhudi zake hazikufaulu.

Vera Sidika na Huddah Monroe
Image: INSTAGRAM//

Vera Sidika amedokeza kuwa hana uhusiano wa karibu na mwanasosholaiti mwenzake Huddah Monroe.

Wakati akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha Maswali na Majibu kwenye mtandao wa Instagram siku ya Alhamisi, mama huyo wa watoto wawili alifichua kuwa zaidi ya muongo mmoja umepita tangu alipozungumza na Huddah mara ya mwisho.

Shabiki mmoja alimuuliza, “Ni lini mara ya mwisho ulizungumza na Huddah?”

Alijibu, “LOL. Huko nyuma mwaka wa 2010."

Vera hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu ugomvi unaodaiwa kuwa kati yake na mfanyibiashara huyo.

Kwa miaka mingi, mastaa hao wawili mashuhuri kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakidaiwa kuwa na uhusiano mbaya.

Katika kipindi cha Maswali na Majibu na mashabiki wake mwaka wa 2021, mke huyo wa Brown Mauzo aliulizwa kwa nini anamchukia sana Huddah, akajibu;

"Kamwe simchukii. Hata mara moja tulikuwa marafiki katika siku za nyuma. Nilipokuwa mpya Nairobi 2009-2010.”

Mwaka wa Oktoba 2019, Vera alisema aliwahi kuwasiliana na Huddah Monroe kufanya biashara, lakini juhudi zake hazikufaulu.

Katika mahojiano na Wasafi Media, mama huyo wa watoto wawili alidokeza kuwa Huddah ndiye alikuwa akimtupia vijembe wala sio yeye.

“Mimi sina beef naye, ninavyomfahamu yeye ndiye ananitupia vijembe kila mara, muda mwingi najua kupuuza, kuna muda nilimtafuta. kufanya biashara naye lakini watu ni tofauti," alisema.

Aliongeza "Siku zote watu watawalinganisha watu maarufu hata kwenye biashara yoyote, nahisi ni kitu cha kawaida, kinatia ladha kwenye game na ni nzuri sana. Sina kawaida ya kujihusisha na biashara za watu wengine maana sijui anahusika na nini na anachofanya."