Babake Akothee ajibu kuhusu kupokea mahari kutoka kwa waume 7 wa msanii huyo

Hapo awali, kumekuwa na tetesi kwamba wanaume kadhaa wamewahi kulipa mahari kwa mwimbaji huyo wakiwa na matumaini ya kumuoa.

Muhtasari

•"Nilimwambia baba yangu kwamba watu kwenye mitandao ya kijamii wanasema amepokea mahari 7 kutoka kwa waume wangu 7, ni kweli?" Akothee alisimulia.

•Mzazi huyo wake alikana kuwahi kupokea mahari kutoka kwa waume wa bintiye, kinyume na inavyodaiwa kwenye mitandao ya kijamii.

na babake mnamo siku ya harusi yake na Omosh
Akothee na babake mnamo siku ya harusi yake na Omosh
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji Esther Akoth almaarufu Akothee amekuwa akifurahia wakati na baba yake katika nyumba yake ya kifahari iliyo eneo la Rongo, Kaunti ya Siaya katika siku chache zilizopita.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 amekuwa akirekodi na kushiriki baadhi ya nyakati zake nzuri na mzazi huyo wake na anaonekana kufurahia sana kila dakika anayoshiriki na mwanamume huyo aliyemlea.

Siku ya Jumamosi, alifichua kwamba alizungumza na babake kuhusu ripoti za kutatanisha ambazo zimeibuka kwenye mitandao ya kijamii siku za nyuma zikidai kuwa takriban wanaume saba wamewahi kulipa mahari katika harakati za kutaka kumuoa.

"Nilimwambia baba yangu kwamba watu kwenye mitandao ya kijamii wanasema amepokea mahari 7 kutoka kwa waume wangu 7, ni kweli?" Akothee alisimulia.

Kulingana na mwimbaji huyo, mzazi huyo wake alikana kuwahi kupokea mahari kutoka kwa wanaume, kinyume na inavyodaiwa kwenye mitandao ya kijami.

"Jibu lake, "Hapana, sijakuona hata ukiwa na mwanamume yeyote," Akothee alisema.

Mama huyo wa watoto watano alishangaa ni kwa nini mzazi wake alikana kamwe kuwahi kumuona na mwanamume yeyote ilhali haijapita hata miezi mingi tangu afunge ndoa na Bw Denis Shweizer almaarufu Omosh katika harusi ya kifahari iliyofanyika jijini Nairobi.

Takriban miezi miwili iliyopita, Akothee alisisitiza kuwa amewahi kuolewa rasmi mara mbili pekee.

Katika taarifa yake, mama huyo wa watoto watano aliweka wazi kwamba ndoa yake na Denis Shweizer almaarufu Bw Omosh  ni ya pili kwa kuwa mahusiano yake mengi ya awali hayakufikia ndoa rasmi.

Akothee aliwataka mashabiki wake kutoamini tetesi nyingi zisizo na msingi wanazoona kwenye mtandao ya kijamii.

"Kwa wafuasi wangu wapya, msiingie kwenye mtego wa watu wenye wivu. Nimeolewa mara moja tu na mahusiano ambayo hayakuweza kufika kwenye ndoa 🤣🤣🤣🤣,hii ni ndoa yangu ya pili," alisema kwenye Instagram.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 alitaja madai mengi kuhusu yeye kuolewa mara kadhaa kuwa uwongo.

Alikana kuwahi kufunga pingu za maisha na wanaume wawili wa Afrika Kusini ambao amewahi kuhusishwa nao katika siku za nyumba huku akibainisha kuwa walikuwa wahusika tu katika video za nyimbo zake.

"Hawa ni vixens kwenye video zangu za muziki. Jisajili kwa chaneli yangu ya YouTube na utazame nyimbo zangu kabla ya kujiaibisha, Oyuech Sweetlove ft diamond na Yuko moyoni ambazo zilirekodiwa  Afrika Kusini," alisema.

Aliongeza, "Wanaume hawa wawili wanaishi Afrika Kusini. Mzungu ameoa na ana familia. Kuweni na adabu.

Akothee alitaka watu wenye nia mbaya dhidi yake waachane naye.

Akothee na mchumba wake Dennis Shweizer almaarufu Mister Omosh walifunga pingu za maisha katika harusi ya kifahari iliyofanyika Windsor Golf Hotel & Country Club, jijini Nairobi mnamo Aprili 10.