"Sina nguvu ya kupigana na ndugu wa damu!" Harmonize amtetea Diamond baada ya kudaiwa kukopi nyimbo

Konde Boy amedokeza kuwa hana kinyongo dhidi ya Diamond na kubainisha hata hana muda na nguvu ya kupigana naye.

Muhtasari

•Diamond amejipata kikaangoni baada ya Wanigeria na baadhi ya Watanzania kumshtumu kwa madai ya kuiba midundo ya wanamuziki wa Nigeria.

•Harmonize alikemea matusi na ukosoaji dhidi ya mwenzake na kuwataka watu kumwacha kila msanii kufanya muziki kwa njia yake.

katika siku za urafiki wao.
Harmonize na Diamond katika siku za urafiki wao.
Image: HISANI

Bosi wa Konde Music Worldwide Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ameonekana kumtetea bosi wake wa zamani Diamond Platnumz katika kipindi ambacho anakabiliwa na tuhuma nzito za kuiba mawazo ya nyimbo za wasanii wengine.

Diamond amejipata kikaangoni baada ya Wanigeria na baadhi ya Watanzania kumshtumu kwa madai ya kuiba midundo ya wanamuziki wa Nigeria, huku kesi ya hivi punde ikiwa ni wimbo wake mpya na Jux ‘Enjoy’ ambao anadaiwa kukopi kibao cha Spyro na Tiwa Savage ‘Who is your Guy.'

Katika taarifa yake siku ya Jumatano, mwimbaji huyo wa kibao ‘Single Again’ aliwataka wasanii wa bongo fleva na mashabiki wao kuungana pamoja na kusaidiana ili kufikia viwango vya juu zaidi.

Harmonize alikemea matusi na ukosoaji dhidi ya mwenzake na kuwataka watu kumwacha kila msanii kufanya muziki kwa njia yake.

“Tuungane pamoja. Tunaweza kuifanya kubwa zaidi. Tumebahatika kuwa waafrika!! Tujifunze kutoka kwa majirani zetu Nigeria. Mambo ya kuvunjana moyo, kuchambana, kuchekana, huyu kakosea huyu, kapatia tu mapungufu mapungufu na kujishushua wenyewe,” Konde Boy alisema kupitia Instagram.

“Biashara kila mtu afanye kwa njia yake!!! Sote tunaenda kileleni,” aliongeza.

Msanii huyo wa zamani wa WCB alidokeza kuwa hana kinyongo dhidi ya bosi wake wa zamani Diamond na kubainisha kuwa hata hana muda na nguvu ya kupigana naye.

"Binafsi sina chochote cha kuthibitisha katika nchi yetu. Kwa kweli sina nguvu ya kupigana na ndugu zangu wa damu. Ndiyo maana naapa kwa Mungu sisi ni wazee sana kwa hilo. Inaweza kuwa biashara ndio, lakini siku zijazo ni nini?,” alihoji.

Kwa muda mrefu, Konde Boy amekuwa akidaiwa kuzozana na Diamond Platnumz na katika siku za nyuma wawili hao wameaonyesha chuki za waziwazi.

Urafiki wa mastaa hao wawili wa Bongo ulisambaratika baada ya Harmonize kuondoka WCB mwaka 2019 na baadaye kuanzisha lebo yake ya muziki ili kukabiliana na maskani yake ya zamani. Wote wawili tangu wakati huo wametupiana shutuma na matusi mazito mazito hadharani na uhusiano wao wa sasa unasemekana kuwa kama maji na mafuta.