Samidoh ajibu baada ya kushtumiwa kuwatelekeza watoto wake

Mwimbaji huyo alishtumiwa kwa kutokuwa mwaminifu na kutelekeza majukumu yake ya ubaba.

Muhtasari

•Hii ilikuwa baada ya Edday Nderitu ambaye kwa sasa anakaa na watoto wake nchini Marekani kuthibitisha kuwa wametangana.

•Edday Nderitu alidokeza kuwa tangu aondoke kwenye ndoa yake amekuwa akiwalea watoto wake watatu peke yake.

Image: INSTAGRAM// SAMIDOH

Mwimbaji wa Mugithi Samuel Muchoki amejibu kwa utani baada ya kushutumiwa kuwa baba asiyekuwepo.

Siku ya Jumamosi, baada ya mahojiano yaliyovuma ya seneta Karen Nyamu na majibu ya Edday Nderitu ambapo alithibitisha kutengana na mwanamuziki huyo na "kumuacha kwa yeyote anayemtaka zaidi", mwanamtandao mmoja alimshutumu kwa kutokuwa mwaminifu na kutelekeza majukumu yake ya ubaba.

"Mbali na ku’cheat wewe ni deadbeat," mtumiaji wa Facebook aliandika chini ya moja ya machapisho yake siku ya Jumamosi.

Mwimbaji wa Mugithi alijibu kwa utani, "Imagine."

Mwimbaji huyo alikuwa amechapisha video liyomuonyesha akiendesha gari katika eneo lisilojulikana. Katika video hiyo, alionekana kufurahia maisha yake sana na kutokuwa na wasiwasi.

"Naendesha kupitia matukio ya Maisha," alisema chini ya video.

Hii ilikuwa baada ya mzazi mwenzake Edday Nderitu ambaye kwa sasa anakaa na watoto wake nchini Marekani kuthibitisha kuwa wametangana.

Katika taarifa yake Jumamosi asubuhi, mama huyo wa watoto watatu aliweka wazi kuwa hayuko kwenye ndoa ya wake wengi na kufichua kuwa alikuwa ameamua kumuacha mume wake wa zaidi ya mwongo mmoja na kuondoka pamoja na watoto wake.

“Siko kwenye ndoa ya wake wengi kama ilivyoelezwa, nilimwacha mume kwa yeyote aliyemhitaji zaidi. Nilifanya uamuzi wa kujiondoa mimi na watoto wangu kutoka kwa mazingira hayo yenye sumu haswa binti yangu kijana ambaye kwa bahati mbaya anapokea moja kwa moja tabia isiyoaminika inayoonyeshwa,” Edday Nderitu aliandika kwenye Facebook.

Aliendelea kudokeza kuwa tangu aondoke kwenye ndoa yake amekuwa akiwalea watoto wake watatu peke yake.

"Nimeweza kushughulikia mahitaji ya watoto wangu hadi sasa bila usaidizi na sijutii hata kidogo," alisema.

Edday alikuwa akijibu matamshi yaliyotolewa na mpenzi wa mzazi mwenzake Samidoh, Karen Nyamu ambaye alidai kuwa bado kuna uhusiano mzuri kati yake na mwimbaji huyo wa Mugithi na kwamba bado huwa wanazungumza licha ya kuwa yuko Marekani kwa sasa.

Akijibu madai kuwa bado anawasiliana na mumewe, Edday alisema, "Kuhusu mawasiliano na simu za video nitaachia hapo kwani watu wengine wanaonekana kuwepo wakati hayo yanafanyika lakini mimi sifahamu. Katika msimu huu mpya wa maisha yangu sihitaji drama yoyote, nahitaji amani tu, natumai kipindi kijacho cha mfululizo huu jina langu litaachwa."

Katika mahojiano na Ala C, Karen Nyamu alisisitiza kuwa mama huyo wa watoto watatu haendi popote kwa kuwa muungano kati yake na Samidoh una nguvu sana.