"Hakuchanga hata 10 bob!" Amber Ray afunguka tukio lililomfanya amchukie Vera Sidika

Amber Ray amekiri kutokuwa na uhusiano mzuri na mwanasosholaiti mwenzake Vera Sidika.

Muhtasari

•Amber Ray alisema kuwa anahisi kama kwamba  mwanasosholaiti huyo mwenzake anaishi maisha ya uwongo mwingi.

•Alidai kuwa Vera Sidika hakuwahi kurudisha upendo ambao rafikiye mmoja aliyeaga alikuwa amemuonyesha katika siku zake za uhai.

Amber Ray na Vera Sidika
Image: INSTAGRAM

 Amber Ray amekiri kutokuwa na uhusiano mzuri na mwanasosholaiti mwenzake Vera Sidika.

Katika mahojiano na Dr. Ofweneke, mama huyo wa watoto wawili aliweka wazi kuwa yeye na Vera hawapendani hata kidogo.

Amber Ray alisema kuwa anahisi kama kwamba mke huyo wa mwanamuziki Brown Mauzo anaishi maisha ya uwongo, jambo ambalo halimpendezi.

“Hatuko sawa. Hatupendani na kwamba ni sawa. Hatupendani. Ninahisi kuwa yeye ni feki sana, wacha niseme hivyo,” Amber Ray alisema.

Mke wa Kennedy Rapudo alifunguka kuhusu tukio ambalo lilimfanya ajenge chuki dhidi ya mwanasosholaiti huyo mwenzake.

Alidai kuwa Vera Sidika hakuwahi kurudisha upendo ambao rafiki yake mmoja aliyeaga dunia alikuwa amemuonyesha katika siku zake za uhai.

"Sababu kwa nini simpendi ni kwa sababu marehemu kaka zangu walikuwepo kwa ajili yake na alipopita, Vera hakuwahi kutokea popote. Hata hakuchanga hata 10 bob,” alisema.

 Amber Ray alibainisha kuwa kulikuwa na haja ya marafiki wa marehemu rafiki yake kushirikiana na kusaidia katika mipango na maandalizi ya mazishi, jambo ambalo kwa mujibu wake, Vera Sidika hakushiriki.

Pia alizungumzia jinsi rafiki yake marehemu alivyosimama na Vera nyakati tofauti kama vile alipokuwa na ujauzito wa mtoto wake wa kwanza.

“Niliona jinsi marehemu rafiki yangu alivyokuwa pale kwa ajili yake na hata kwenye baby shower yake ya kwanza, marehemu rafiki yangu alimpea karibu kila kitu. Akamlipia bills za hospital. Kwa mtu ambaye amefanya mengi kwa ajili yako, angalau kuwa na utu. Kuwa wa kweli, "alibainisha.

Kufuatia hayo, alisema kuwa tukio hilo lilimfanya kukomesha urafiki na ushirikiano wowote na mwanasosholaiti huyo mwenzake.

Kwa muda sasa, wanasosholaiti hao wawili ambao sasa wanatunza watoto wachanga wameonyesha uhusiano wao mbaya hadharani. Mapema mwaka huu, Vera alimshutumu Amber kwa kuiba wazo lake la kufichua jinsia ya mtoto wake alipofanya karamu yake kutumia chopa. 

"Walitaka kufichua jinsia na chopper pia. Mipango ilibadilika dakika ya mwisho kwa sababu nilichapisha yangu na ilivuma kwa siku tatu.

“Ilibidi watafute plan B kwa sababu sasa ingekuwa wazi sana juu Chopper ilikuwa tayari ipo. Ilibidi watafute tu njia ya kuitumia.

"Aliambia mpangaji anataka kucopy sherehe yangu yote ya jinsia na hufanya hivyo kabla ya maonyesho yangu kwenye TV,” Vera alidai. 

Amber hata hivyo alikanusha madai hayo akisema kuwa wazo hilo la kufichua jinsia kutumia chopa lilianzishwa mwaka wa 2008 na Jenna Karvunidis na yeyote ambaye amelifanya hilo baada ya hapo alikuwa akimuiga tu.