Kuwa na mke mmoja pekee kunaweza kumzuia mtu kwenda mbinguni - Bahati

Bahati alihoji ni wapi imeandikwa kwenye Biblia kwamba ni dhambi kuoa zaidi ya mke mmoja.

Muhtasari

•Mwimbaji Bahati alidokeza kwamba kuwa na wake wengi hakuwezi kumzuia mwanamume kwenda mbinguni.

•Bahati alitumia mfano wa Sulemani na jinsi alivyokuwa na wake wengi na bado kuna uwezekano mkubwa yuko mbinguni.

Diana Marua na mumewe Bahati
Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mwanamuziki mashuhuri wa nyimbo za mapenzi Kelvin Kioko almaarufu Bahati alishiriki mazungumzo ya wazi na mmoja wa wafanyikazi wake, Baite ambapo walijadili suala la ndoa ya wake wengi.

Katika mazungumzo hayo yaliyoshirikiwa kwenye chaneli ya YouTube ya Diana Marua, wanaume hao wawili walionekana kutetea ndoa ya wake wengi kwa kutumia Biblia kama marejeleo.

Bahati alidokeza kwamba kuwa na wake wengi hakuwezi kumzuia mwanamume kwenda mbinguni, na badala yake, kuwa na mke mmoja huenda kunaweza kuziba njia ya mtu kuenda mbinguni.

“Mi naona kitu kimoja kinaweza kufanya wanaume wasiende mbinguni ni hiyo kuchukua bibi mmoja. Tunaweza kufika tuambiwe ‘mbona mimi niliruhusu David na Solomon wakuwe na mabibi wengine na nyinyi mko na mmoja?’” Bahati alimwambia Baite.

Baba huyo wa watoto wanne alibainisha kuwa kuna uwezekano kuwa wale ambao wana wapenzi wengi ndio watakaofika mbinguni.

“Unajua watu wanaweza kudhani wale watu wanachepuka ndio hawataenda mbinguni, upate hao ndio wataenda mbinguni. Sasa tutafanya nini tukifike huko,” alisema.

Muimbaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alihoji ni wapi imeandikwa kwenye Biblia kwamba ni dhambi kuoa zaidi ya mke mmoja.

Alitumia mfano wa Sulemani kutoka katika Biblia na jinsi alivyokuwa na wake wengi na bado kuna uwezekano mkubwa kwamba sasa yuko mbinguni.

Wakati huo huo alimsifu Mfalme huyo wa kale wa Israeli kwa kuweza kuwadhibiti wake wote zaidi ya mia saba aliokuwa nao na kubainisha kuwa haijawahi kuwa rahisi kuishi na mke hata mmoja.

"Kama kuishi na bibi moja ni stress, watu mia saba," alisema.

Kwa sasa Bahati yuko kwenye ndoa na Diana Marua. Wawili hao waliingia kwenye uhusiano zaidi ya nusu muongo uliopita na tayari wana watoto watatu pamoja. Hata hivyo, bado hawajafunga ndoa rasmi.

Mwezi uliopita hata hivyo, Bahati alimchumbia Diana Marua na kutangaza kwamba watafunga ndoa mwishoni mwa mwaka huu.

Wakati akichukua hatua hiyo kubwa, Bahati alibainisha kuwa amekamilisha hatua zote muhimu kuelekea ndoa na sasa yuko tayari kuifanya rasmi.

"Umenipatia moyo wako. Kusema kweli kutoka ndani ya moyo wangu, siichukulii virahisi. Kitu kimoja ambacho ninataka sana kufanya mwaka huu, nataka tu kuhakikisha nimefanya sawa, najua nimeenda kwa familia yako kwa utambulisho lakini mwaka huu nataka tufanye harusi ya kweli na nataka kukuoa," Bahati alimwambia mchumba wake.

Kwenye ukurasa wake wa Instagram, mwanamuziki huyo alitangaza tarehe 12 Desemba kuwa siku ya harusi yao.

"Alisema ndiyo.  Na natangaza rasmi kwamba Desemba 12 ni siku ya harusi yetu," alisema.