Mwanamke amfukuza mpenzi mume mwenye boma akirudi baada ya miaka 17 - video

"Mzee wangu alipotoweka, nilikaa miaka 5 uvumilivu ukanishinda... nilipata kijana Mnyarwanda tukaishi naye kwangu na tukazaa mtoto mmoja, ni kijana mzuri alikuwa ananisaidia kulea watoto wengine..."

Muhtasari

• Baada ya kupata taarifa za ujio wa mumewe, alilazimika kumwambia kijana yule kwamba baba mwenye boma amerudi.

• Kijana yule alielewa na kujitoa na kwenda kupangisha maisha yake kwingine akiahidi kuendelea kumshuhulikia mwanawe.

Image: Screengrab

Mwanamke mmoja katika kaunti ya Kakamega amewashangaza wengi baada ya kukiri kwamba alilazimika kumfukuza mpenzi wake waliyeishi naye hadi kuzaa mtoto mmoja naye.

 Mwanamke huyo ambaye hakutambuliwa kwa jina alielezea runinga ya Citizen kwamba alilazimika kutafuta mpenzi wa kumpa joto baada ya mume wake kuondoka nyumba bila kurudi kwa miaka 17.

Alisema kwamba mume wake alipoondoka nyumbani, alijisatiti kuvumilia kwa takribani miaka 5 lakini uvumulivu ukamshinda, na wakwe zake nyumbani walikuwa wanamuonya vikali dhidi ya kuleta mtu katika boma hilo, wakiamini kwamba mzee wake angerudi tu.

“Sasa nilikaa karibu miaka 5, nikasema nimevumilia vya kutosha sitaweza. Na mamangu bado alikuwa ako hai, baba mkwe ako hai. Sasa wakawa wakali, nikasikia amri zao kidogo. Walikuwa wananikataza hawataki kuwa na mtu hapo kwa boma, lakini kweli yenyewe mama alimalizia kugonjeka na kufa, na hapo ndio nilipata mtu,” mama huyo alisimulia.

Alisema kuwa alipata kijana ambaye ni raia wa Rwanda na waliishi naye akichukua jukumu kama la mume wake, kumsaidia kuwalea watoto wengine na mwisho wa siku akamalizia kuzaa naye mtoto mmoja pia.

Mama huyo alisema kijana huyo alikuwa mtu mzuri wa kukaa naye kwani alikuwa hata anawashughulikia masuala ya utaalamu wa vinywani lakini pia kuwalipia watoto wake karo ya shuleni.

“Vile nilisikia kwamba mume anarudi, nilishtuka sana. Lakini pia yeye [mpenzi mpya] sikumficha, nilikaa na yeye kwa upole na nikamwambia si kwa ubaya sikufukuzi lakini mwenye boma amerudi, lazima tutampa heshima kwa sababu hili ni boma lake. Na yeye alinielewa,” mama huyo aliendelea kusimulia.

Zaidi ya hayo kijana alikwenda akapanga nyumba yake lakini kulikuwa na suala moja la kuwaunganisha bado – mtoto.

“Nilimwambia kweli enyewe tumezaa na wewe mtoto, na sidhani kama mzee wangu atamshuhulikia huyu mtoto. Mwenyewe ujikakamue na mtoto wako, akakubali mtoto wangu mimi nitamshughulikia lakini tupatie mzee wa boma heshima yake kwa sababu nilikuja kama sijui kama ako hai ama amekufa,” alimnukuu.

Mzee wa boma aliporudi, alifanyiwa tambiko la kukaribishwa nyumbani na hata kuombewa, na mama huyu alieleza furaha yake pamoja na ya watoto wake.

“Kwa kweli yenyewe tulikuwa na furaha, tumesikia roho ndani ya mioyo yetu, hadi watoto wake wamefurahia kwa sababu walikuwa wanajua sisi hatuna baba, tuko tu na mama peke yake. Wacha tu Mungu aitwe Mungu sababu hata mimi mwenyewe nilikuwa nimesema huyo ameenda,” alisema.