Akothee hatimaye afichua kwa nini alitengana na Nelly Oaks

Mwimbaji huyo aliweka wazi kuwa ni uhusiano wa kimapenzi tu na Nelly Oaks ambao uliisha lakini urafiki wao ulisalia.

Muhtasari

•Akothee alifichua kuna mambo mengi  yaliyomchochea yeye na Nelly Oaks kwenda njia tofauti katika masuala ya kimapenzi.

•Akothee alibainisha kuwa ukaribu wake hata baada ya kutengana na Nelly Oaks hauna madhara yoyote kwenye ndoa yake.

Nelly Oaks na Akothee
Nelly Oaks na Akothee
Image: INSTAGRAM//NELLY OAKS

Mwimbaji na mjasiriamali Esther Akoth almaarufu Akothee amezungumza kuhusu kutengana kwake kimapenzi na meneja wake Nelson Oyugi almaarufu Nelly Oaks.

Katika mahojiano ya wazi na Dr. Ofweneke, mama huyo wa watoto watano alifichua kuwa kuna mambo mengi ambayo yalimchochea yeye na mwanaume huyo kutoka kijijini kwao kwenda njia tofauti katika masuala ya kimapenzi.

Akothee alidokeza kuwa pia hakuwa sawa kisaikolojia wakati wa kutengana na meneja huyo wake zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

"Tulipoenda njia tofauti, kuna mambo mengi ambayo yalisababisha tushindwe kuendelea. Pia nilikuwa nikipitia mengi lakini watu hawajui kuwa Nelly amekuwepo kwa ajili yangu,” Akothee alisema.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 alimsifu Nelly Oaks kwa ukakamavu wake akidokeza kwamba si wanaume wengi wangestahimili kuwa naye kama alivyofanya.

"Tulikaa pamoja kwa miaka minane, 24/7. Alikuwepo, nilikuwa na wanaume wengine watatu maishani mwangu, nilikuwa na baba watoto wangu wawili pamoja nami. Nilikuwa na mshirika wangu wa biashara, kisha nilikuwa na Nelly Oaks pamoja nami. Na kisha nilikuwa na watoto wangu watano, pia kulikuwa na Esther, Madam Boss na Akothee. Mnafaa kumpigia makofi huyu jamaa,” alisema.

Mwimbaji huyo alibainisha kuwa ukaribu wake hata baada ya kutengana na Nelly Oaks hauna madhara yoyote kwenye ndoa yake.

Aliweka wazi kuwa hata kabla hata ya kuingia kwenye uhusiano na mumewe Denis Shweizer almaarufu Omosh, tayari alikuwa amemweleza kuhusu mambo mengi kuhusiana na maisha yake yakiwemo mahusiano yake ya awali.

“Kwa kawaida huwa sina cha kuficha kwa sababu sitaki utafute chochote cha kutumia dhidi yangu. Nitawaambia wapenzi wa zamani wangu wote, nitakwambia barabara zote nilizopita, nitakwambia watoto wote niliozaa. Ili ujue chochote unachojiletea. Kwa hivyo ni aidha uanzishe kutoka hapo, au ujiondoe kutoka hapo. Afadhali unitupe siku ya kwanza kabla ya kula keki yangu. Huli halafu huko mbele unasema hukujua,” alisema.

Akothee alidokeza kwamba alikutana na mumewe mzungu kipindi kifupi baada ya kutengana na Nelly Oaks. Wawili hao walikuwa wamechumbiana kwa miaka kadhaa kabla ya mwimbaji huyo kuthibitisha kutengana kwao mapema mwaka jana.

Alifichua kwamba wakati wa kutengana kwao, alikumbwa na msongo wa mawazo, hali ambayo anasisitiza haikutokana na mahusiano yao.

"Nilikuwa na mambo mengi yanayoendelea. Nilihisi mahusiano hayo pia yalikuwa yakinilemea,” alisema.

Mwimbaji huyo aliweka wazi kuwa ni uhusiano wa kimapenzi tu na Nelly Oaks ambao uliisha lakini urafiki wao haukuisha.

"Kwa Nelly Oaks naona kaka, baba, rafiki. Inapita mambo haya yote ambayo watu wanasema. Tulijenga muungano,” alisema akidokeza kwamba hakuna njia ambayo angemchukia mpenzi huyo wake wa zamani.