Harmonize afunguka kuhusu kupata mtoto wa pili

Zulekha Rajabu almaarufu Zuuh Konde ni mtoto pekee wa Harmonize.

Muhtasari

•Staa wa Bongo, Harmonize amethibitisha kuwa bado hayuko tayari kabisa kupata mtoto mwingine.

•Konde Boy alibainisha kuwa binti yake anakaribia sana kufanana na mama yake, jambo ambalo tayari limemfanya kuridhika.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Staa wa Bongo, Harmonize amethibitisha kuwa bado hayuko tayari kabisa kupata mtoto mwingine.

Wakati akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha Maswali na Majibu kwenye mtandao wa Instagram, baba huyo wa mtoto mmoja alithibitisha kuwa kwa sasa ameridhishwa na bintiye wa pekee, Zuuh Konde.

Konde Boy alibainisha kuwa binti yake anakaribia sana kufanana na mama yake, jambo ambalo tayari limemfanya kuridhika.

Jumanne, shabiki mmoja alimuuliza, “Una mpango wa kupata mtoto mwingine mbali na Zuuh Konde?”

Bosi huyo wa Konde Music Worldwide alijibu, “Siko tayari. Zuuh kweli anafanana na Mama Konde. Kwa hiyo siko tayari.”

Zulekha Rajabu almaarufu Zuuh Konde ni mtoto pekee wa Harmonize.

Malkia huyo mdogo mwenye umri wa miaka mitano alizaliwa takribani miaka mitano iliyopita wakati staa huyo wa bongo fleva alikuwa na mahusiano ya kipindi kifupi na mfanyibiashara wa Tanzania, Official Shanteel.

Mnamo mwezi Mei, Zuuh Konde alisherehekea miaka mitano tangu alipoletwa humu duniani na mama yake Official Shanteel.

"Nakupenda. Mungu wangu akulinde Konde Queen. Heri ya siku ya kuzaliwa boss lady," Harmonize alimsherehekea bintiye.

Shanteel ambaye ni mfanyibiashara wa samani pia alimsherehekea bintiye na kumhakikishia kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

"Happy birthday mwanangu kipenzi nakupenda sana @zuuh_konde," alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mapema mwaka huu, Harmonize alidokeza kuhusu hatua ya binti  huyo wake wa pekee kujiunga na shule ya chekechea.

Konde Boy alionyesha video ya yeye, baby mama wake, bintiye na mwalimu baada ya kulipa karo ya shule na kuandika:

"Nifanye nijivunie. Niko hapa kwa ajili yako. Baba anakupenda, sawa ni wakati wa shule," aliandika chini ya video hiyo.

Official Shanteel alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Harmonize wakati mwanamuziki huyo alikuwa bado akichumbiana na Sarah Michelloti. Uhusiano huo wa kipindi kifupi ulifanya wawili hao kujaliwa mtoto mmoja  wa kike pamoja, Zulekha Nasra (Zuuh Konde) na pia ulivunja ndoa ya bosi huyo wa Kondegang na Sarah.

Mwaka wa 2021, Harmonize alipokuwa akizindua albamu yake  'High School' alifunguka kuhusu utata uliozingira kuzaliwa kwa bintiye.

Mwimbaji huyo alifichua kwamba kuzaliwa kwa mtoto huyo ndicho chanzo cha kuvunjika kwa ndoa yake ya kwanza na Sarah Michelloti.

Harmonize alisema ndoa yao ya miaka minne ilianza kusambaratika wakati mpenzi wake alikuwa amesafiri kuenda kwao na baada ya kuwa pweke kwa muda akapata majaribu ya kutembea na mwanadada aliyemzalia mtoto.

"Ilikuja kipindi akawa anasafiri kuenda kwao. Nilikuwa Tanzania na kama unavyojua umbali wa mapenzi unapokuwa nikaishia kutembea na mwanamke ni mama Zuuh sasa hivi. Kwa mipango ya mwenyezi Mungu nikamfanya mjamzito." Harmonize alisema.

Konde Boy alifichua kwamba Shanteel alikuwa na wasiwasi kuhusu ujauzito huo na hata alikuwa tayari kuutoa ila akamkataza.

Alisema kuwa alikubali majukumu na akahudumia ujauzito ujauzito hadi mtoto alipozaliwa.