Harmonize ageukia pombe baada ya Kajala kumwaga mtama kuhusu uhusiano wao uliovunjika

Konde Boy alikuwa ametishia kufunguka zaidi kuhusu utapeli wa ex wakeKajala wakati akilewa.

Muhtasari

•Mara baada ya mahojiano ya Kajala na waandishi wa habari, Konde Boy alitangaza kuwa yuko tayari kulewa na hata akaendelea kukata maji.

•Wanahabari wa Tanzania walimsukuma sana Kajala kusema ukweli wake wakati wa mahojiano ya Jumatano.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Siku ya Jumatano, muigizaji wa Tanzania Fridah Kajala Masanja alivunja ukimya kuhusu masuala mbalimbali ambayo alihitajika kufafanua.

Kajala alifanya kikao na mwandishi wa habari ambapo alitoa mwanga kuhusu mahusiano yake yaliyovunjika na mwimbaji Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize na pia akajibu baadhi ya tuhuma ambazo bosi huyo wa Kondegang alimzushia siku chache zilizopita.

Wiki iliyopita, Konde Boy aliachia wimbo ‘Dear Ex’ ambapo alifunguka baadhi ya mambo kuhusu uhusiano wake uliovunjika na Kajala na pia akamshutumu mama huyo wa mtoto binti mmoja kwa kuwa tapeli. Zaidi ya hayo, mwanamuziki huyo pia alidai kuwa mpenzi huyo wake wa zamani amepungua sana baada ya kutengana naye mwaka jana.

"Hello dear EX, nimepata tetesi za kwamba unanisema ili nionekane sio mwema, pengine una stress, maana umekonda mwepesi, ukimya si ukilema ila nachunga vya kusema, maana niliubeba msalaba nikawa mi ndo mama ndo baba nikajichanga tujaze kibaba mbona hausemi?" Harmonize aliimba.

Aliendelea, “"Kiume nilishukuru nikapangusa m*tak* nikakuacha uende ukawe huru, Range na duka ni vyako nibaki na m*kend*."

Mwimbaji huyo wa kibao ‘Single Again’ aliendelea kutishia kufunguka zaidi kuhusu utapeli wa Kajala siku moja baada ya kubugia chupa kadhaa za tembo na kulewa.

Siku ya Jumatano, mara baada ya mahojiano ya Kajala na waandishi wa habari, Konde Boy alitangaza kuwa yuko tayari kulewa na hata akaendelea kukata maji.

 “Ohooo!!! Pombe zimeanza kuingia,” alitangaza katika moja ya taarifa zake kwenye mtandao wa Instagram.

Katika sasisho lingine, alidokeza kuwa tayari alikuwa amelewa.

"Alooo nimelewa!!!"

Mashabiki wake walimsubiri sana staa huyo wa bongo fleva aanze kutema ukweli wake lakini kwa bahati mbaya alinyamaza baada ya kutangaza kuwa tayari amelewa.  Bado hatufahamu vyema ikiwa alifikiria upya kuhusu tishio lake la awali au alibugia pombe nyingi hadi akazima.

Siku ya Jumatano, wanahabari wa Tanzania walimsukuma sana Kajala kusema ukweli wake wakati wa mahojiano lakini mama huyo wa mtoto mmoja alijibu tu kuhusu masuala kadhaa ambayo alikuwa tayari kuyazungumzia.