Kajala afunguka wema wa Harmonize kwa babake, ajibu kupata dili kutokana na vita vyao

Kajala amethibitisha kuwa ni kweli Harmonize alimsaidia baba yake Bw Masanja.

Muhtasari

•Muigizaji huyo mkongwe wa filamu bongo alitakiwa kujibu kuhusu iwapo Harmonize aliwahi kumsaidia mzazi huyo wake.

•Alibainisha kuwa alipata umaarufu hata kabla ya mwimbaji huyo ambaye ni mdogo wake kwa miaka kadhaa kuingia mjini.

Harmonize na mchumba wake Kajala Masanja
Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Aliyekuwa mpenzi wa Harmonize, muigizaji Fridah Kajala amethibitisha kuwa ni kweli msanii huyo wa bongo fleva alimsaidia baba yake Bw Masanja.

Wakati akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano, muigizaji huyo mkongwe wa filamu bongo alitakiwa kujibu kuhusu iwapo Harmonize aliwahi kumsaidia mzazi huyo wake.

Katika majibu yake, Kajala alibainisha, "Ndiyo kwa hakika, aliwahi."

Kajala alikuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa ushirikiano wake na kampuni ya Luna Sanitary Pads ambapo alitangazwa kama balozi mpya wa chapa hiyo.

Katika mahojiano hayo, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 40 pia alijibu madai ya kupata dili za matangazo kutokana na umaarufu uliotokana na uhusiano wake na Harmonize uliovunjika na vita vya maneno vinavyoendelea kati yao.

Katika jibu lake, mama huyo wa binti mmoja alibainisha kuwa alipata umaarufu hata kabla ya mwimbaji huyo ambaye ni mdogo wake kwa miaka kadhaa kuingia mjini.

“Nadhani mimi nimeanza kujulikana kama hata Harmonize hayupo mjini. Kwa hivyo huwezi kuniambia kwa ajili ya kubishana na Harmonize ndiyo nimepata madili,” alisema.

Mama huyo wa mwanamitindo Paula Kajala pia alikanusha madai kuwa tayari ameshauza gari aina ya Range Rover ambalo alinunuliwa na staa huyo wa bongo wakati alipokuwa akimuomba msamaha mapema mwaka jana akilenga kufufua mahusiano yao ambayo yalikuwa yamevunjika mwaka  wa 2021.

“Range sijaiuza, Range ipo. Kuhusu kutumia Toyota, ni kweli mara nyingi natumia gari la Paula. Huwa nahisi inakuwanga very comfortable kwa sababu lile (Range) likiwa na jina kuna sehemu huwa nataka kwenda na sitaki kuitwa Kajala. Kwa hiyo mara nyingi natumia gari la Paula. Hata ni kutumia Toyota ama ST, ni gari,” alisema.

Kuhusu kuwa na nambarisiri za akaunti zote za benki za mwanamuziki huyo, Kajala alibainisha kuwa kila mtu katika Kondegang anazo kwani mwimbaji huyo wa kibao ‘Single Again’ huwa anamtuma yeyote kwenda kununua au kupata kitu kwa kutumia kadi zake za mkopo.

Pia alijibu kuhusu kupokea 10% ya mapato ya staa huyo wa bongo kutokana na shoo na dili zote alizofanya ambapo aliweka wazi kwamba alipata kitu katika miezi miwili ya mwisho ya mahusiano yao.

“Tulivyokuwa tunaanza, ilikuwa sio kweli. Alafu miezi miwili kabla ya mimi na yeye kuachana ndio alinipea hiyo asilimia kumi. Alafu tutakuja tukaachana. Kama yeye alisema ni asilimia kumi, basi ni asilimia kumi,” alisema Kajala.

Kajala alikuwa akijibu tuhuma zilizoibuliwa na bosi huyo wa Konde Music Wordwide wiki jana kwenye wimbo wake 'Dear Ex' na posti kadhaa ambazo alichapisha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.