Samidoh ajibu vikali baada ya kushutumiwa kwa kutelekeza mkewe na watoto wake

Samidoh amejibu baada ya mwanadada kumwambia haoni chochote kizuri kwake tangu alipodaiwa kutema familia yake.

Muhtasari

•Shabiki alimtaja Samidoh kama mtu aliyeshindwa kabisa huku akimshutumu kwa kumtema mkewe na watoto wake.

•Katika jibu lake, Samidoh alimtaka shabiki huyo azingatie mambo yake mwenyewe na kuachana naye.

Image: INSTAGRAM// SAMIDOH

Mwimbaji wa nyimbo za Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh alionekana kutoridhika baada ya mtumiaji wa mtandao kumshambulia akimshutumu kwa kutelekeza familia yake.

Chini ya moja ya machapisho yake kwenye Facebook, mwanadada mtumizi wa mtandao huo wa kijamii alimtaja kama mtu aliyeshindwa kabisa huku akimshutumu kwa kumtupa mkewe na watoto wake.

Mwanadada huyo alimtaka mwanamuziki huyo aeleze jinsi anavyoweza kuishi vizuri wakati akidaiwa kujitenga na familia yake.

“Sioni kitu kizuri kwa huyu mwanaume tangu amuache mke na watoto! Aliyeshindwa kabisa! Je, unajisikiaje kuwaacha tu watoto wako wakitangatanga ulimwenguni kwa sababu ya tabia yako isiyodhibitiwa? Unapataje hata usingizi? Unakaaje na kula kwanza?” Mtumiaji wa Facebook kwa jina Mary Wangechi aliandika.

Katika jibu lake, Samidoh alimtaka shabiki huyo azingatie mambo yake mwenyewe na kuachana naye.

Mwanamuziki huyo kwa kejeli alimtaka shabiki huyo aondoke kwenye ukurasa wake na kwenda kutafuta mambo mazuri kwenye ukurasa wa mumewe.

“Heheh, sasa simama polepole upeleke kiherehere kwa page ya bwanako hapo ndipo kuna kila kitu kizuri sawa?” Samidoh alijibu.

Haya yanajiri wakati mke wa kwanza wa mwanamuziki huyo wa nyimbo za Kikuyu, Bi Edday Nderitu pamoja na watoto wao watatu wanaaminika kuwa nchini Marekani. Wanne hao wamekuwa katika nchi hiyo ya Magharibi mwa dunia kwa miezi kadhaa sasa baada ya kuondoka Kenya mapema mwaka huu.

Mwezi uliopita, Edday aliweka wazi kuwa alimuacha mume wake ili kuwa na mwanamke ambaye alionekana kumtaka zaidi.

"Wacha nifafanue mambo machache ambayo yalishirikiwa mtandaoni na sio sahihi. Siko kwenye ndoa ya wake wengi, kama ilivyoelezwa nilimuacha mume kwa yeyote aliyemhitaji zaidi,” Edday alisema kupitia Facebook.

Aliongeza, "Nilifanya uamuzi wa kujiondoa mimi na watoto wangu kutoka kwa mazingira hayo yenye sumu, haswa binti yangu kijana ambaye kwa bahati mbaya anapokea moja kwa moja tabia isiyoaminika iliyoonyeshwa."

Mama huyo wa watoto watatu alibainisha kwamba hajutii uamuzi wa kugura ndoa yake ya zaidi ya mwongo mmoja na akaweka wazi kuwa ameweza kuendelea kuwalea watoto wake bila usaidizi wowote.

Pia alizungumzia madai ya Karen Nyamu kwamba yeye na watoto wake huwa wanawasiliana na mwimbaji Mugithi kwa simu.

"Kuhusu mawasiliano na simu za video, nitaachia hapo kwani baadhi ya watu wanaonekana kuwepo wakati hilo linafanyika lakini mimi sifahamu. Katika msimu huu mpya wa maisha yangu, sihitaji drama yoyote, nahitaji amani tu, natumai kipindi kijacho cha mfululizo huu jina langu litaachwa,” alisema.

Baada ya mkwe wake kuhama Kenya, Samidoh amekuwa akionekana mara nyingi akiwa pamoja na seneta Karen Nyamu na mapenzi kati ya wazazi wenza hao yameonekana kunoga zaidi katika kipindi hicho.

Image: FACEBOOK// SAMIDOH