Ningejua mke ana nguvu kuniliko nisingemuoa - Mume anayepigwa na mke alia kwa majuto

Katika miaka 4 ambayo wamekuwa kwenye ndoa na mke wake, tayari amepigwa mara kadhaa na kwa mara 7 amejaribu kufungasha virago na kuondoka lakini mke anamzuia vikali kumuonya.

Muhtasari

• Chapisho hilo lilivutia maoni mengi baadhi wakimlaumu kwa kuendelea kuwa mtumwa wa ndoa hali ya kuwa anadhulumiwa.

Mwanamume mwenye huzuni na mfadhaiko.
Mwanamume mwenye huzuni na mfadhaiko.
Image: Maktaba

Mwanamume mmoja ambaye anapitia wakati mgumu kwenye ndoa yake amepeleka malalamiko yake kwenye jukwaa moja la mitandaoni linalolenga kuangazia matatizo ya watu kwa ahadi ya kubana majina yao ili wasije wakadhuhakiwa na wanaowajua.

Mwanamume huyo alilia kwa majuto makubwa kwamba anapiga na mke wake kila mara anapomchukiza kwa kitu kidogo tu, jambo ambalo limemfanya kuiona ndoa yake kama shubiri wakati rafiki zake wanaisifia kama bustani la maua mazuri.

Mwanamume huyo ambaye jina lake lilibanwa alifichua kwamba mke wake ni mtu mwenye hasira na anamdunda kila wakati, huku akijuta kwamba laiti angefahamu mapema kuwa mke ana nguvu kumliko basi asingefanya udhubutu hata wa kumuoa.

Alisema kwamba katika miaka minne ambayo wamekuwa kwenye ndoa na mke wake, tayari amepigwa mara kadhaa na kwa mara 7 amejaribu kufungasha virago na kuondoka lakini mke anamzuia vikali akimuonya dhidi ya kufanya uamuzi wa kumtoroka.

“Mke wangu ananipiga kila baada ya kumghasi kidogo tu. Wakati mwingine huwa natoroka na kujificha jikoni kukwepa kipigo chake. Tayari nimejaribu mara 7 kufungasha vilivyo vyangu na kuondoka katika nyumba yangu katika miaka minne ya ndoa yetu,” alisema.

“Huwa siongei wakati amekasirika. Laiti ningalijua kwamba ana nguvu kunishinda nisingekubali kuweka miadi ya ndoa na yeye…” alimaliza kwa majuto.

Chapisho hilo lilivutia maoni mengi baadhi wakimlaumu kwa kuendelea kuwa mtumwa wa ndoa hali ya kuwa anadhulumiwa.

Wengine pia walimdhihaki kwa kudhalilisha hadhi ya uanaume wakisema kuwa mwanamume kamili wa Kiafrika hawezi kulaza damu hivi hivi tu akidundwa na mwanamke kama ngoma iliyowambwa.

Hata hivyo, kuna wale ambao walitoa wito kwa mamlaka husika na mashirika na kutetea haki za binadamu wakisema kwamba dunia ya sasa imeweka uzingatifu mkubwa kwa visa vya wanawake kudhulumiwa kwenye ndoa lakini hakuna anayejitolea kuzungumzia suala la wanaume kudhulumiwa vile vile kwenye ndoa kwa vipigo na mateso kutoka kwa wapenzi wao.