Karen Nyamu, mzazi mwenzake DJ Saint Kevin wamsherehekea binti yao kwa njia ya kupendeza

Katika ujumbe wake, Saint aliizungumzia jinsi binti yake anavyosisimua maisha yake na ya watu wengine karibu naye.

Muhtasari

•Kulingana na Nyamu, malkia huyo mdogo aliomba kuabiri SGR na seneta huyo alibainisha kuwa pia yeye alifurahia sana safari ya treni.

•DJ Saint alishiriki picha yake nzuri na Tiana na kwenye sehemu ya maelezo, alieleza upendo wake mkubwa kwake.

Karen Nyamu na mzazi mwenzake DJ Saint Kevin
Image: HISANI

Mtoto wa kwanza wa Seneta wa Kuteuliwa Karen Nyamu, Tiana aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa jana, Agosti 24.

Ili kumsherehekea bintiye akitimiza umri wa miaka tisa, mwanasiasa huyo alitimiza matakwa yake ya siku ya kuzaliwa ya kupanda treni ya SGR.

Kulingana na seneta Karen Nyamu, malkia huyo mdogo aliomba kuabiri SGR na seneta huyo alibainisha kuwa pia yeye alifurahia sana safari ya treni.

“Kwa hiyo juzi nilipanda SGR kwa mara ya kwanza kabisa, shukrani kwake (Tiana). Ilikuwa ombi lake la siku ya kuzaliwa. Niliipenda,” Karen Nyamu aliandika chini ya video yake na bintiye huyo ndani ya treni ya SGR aliyoichapisha kwenye Instagram.

Seneta huyo wa UDA aliendelea kukiri upendo wake mkubwa kwa mzaliwa huyo wake wa kwanza na kukiri jinsi anavyojivunia kuwa mzazi wake.

"Siku ya kuzaliwa yenye furaha kwa msichana mzuri zaidi, mwenye talanta zaidi, mwenye furaha zaidi na mwenye upendo zaidi. Najisikia heri kuwa mama yako mtoto,” alisema.

Karen Nyamu sio mtu pekee maalum katika maisha ya Tiana ambaye alimsherehekea hadharani, baba ya msichana huyo mdogo, mcheza santuri DJ Saint Kevin pia alimwandikia ujumbe mtamu wa kuadhimisha siku yake maalum.

Katika ukurasa wake wa Instagram, mburudishaji huyo alishiriki picha yake nzuri na Tiana na kwenye sehemu ya maelezo, alieleza upendo wake mkubwa kwake.

Katika ujumbe wake, Saint aliizungumzia jinsi binti yake anavyosisimua maisha yake na ya watu wengine karibu naye.

"Heri ya kuzaliwa kwa binti yangu wa kifalme ambaye hunifanya nione maisha katika rangi kamili! Unaongeza furaha kwa kila mtu unayekutana naye na leo tunasherehekea uzuri wa kufurahisha ulio nao. Nakupenda mtoto wangu,” DJ Saint Kevin aliandika.

DJ Saint ndiye baba wa mtoto wa kwanza wa Karen Nyamu. Wawili hao walichumbiana kwa kipindi kabla ya kwenda njia tofauti.

Mwaka jana, mcheza santuri huyo alizungumza kuhusu jinsi mahusiano yao ya miaka kadhaa yalivyokuwa sumu.

Akiongea kwenye ukurasa wake wa Instagram,  alisema kuwa kazi yake kama DJ ilichangia uhusiano wao mbaya.

“Kama Dj huwa natangamana na wanawake mara kwa mara, shabiki wa kike anaweza kupanda jukwaani na kukupa busu shingoni huku akiomba wimbo na Karen alishindwa kuvumilia. Hata kama hatasababisha drama kwenye hafla hiyo, tunapoingia kwenye gari kurudi nyumbani, ni msomo mpaka nyumbani," alifichua.

DJ Saint aliongeza kuwa walizozana kila siku na kusababisha mvutano ambao ulisababisha kutengana kwao.

"Ilikuwa ni vita baada ya vita, na mimi kuamua kuondoka tulikuwa tumefikia hatua ya kutorudi nyuma. Kila mara ilikuwa mabishano na niliona sio sawa kwa sisi kumlea mtoto wetu katika mazingira hayo. Niliamu kumpa nafasi na ikawa sawa. Ilikuwa ni sumu, kila siku mapigano," Dj Saint aliendelea kusimulia.

Alisema kwamba Karen ni mama mzuri na akabainisha kuwa wanashirikiana vizuri katika malezi ya binti yao.

Akizungumza katika mahojiano na Alibaba kwenye Radio Jambo mwaka wa 2021, baba huyo wa watoto wawili alisema alikutana na Karen kwenye hafla ambayo alikuwa akitumbuiza kama mcheza santuri.

”Nilikutana na Karen kabla ya kuwa mwanasiasa. Alikuwa wakili na nilikuwa kwenye hafla ya DJ,” alisema.

Baada ya kutengana, Karen baadaye alikutana na mwimbaji Samidoh na wakabarikiwa na watoto wawili pamoja.