Hongera! Mwimbaji Nyota Ndogo apongezwa baada ya kudokeza anatarajia mtoto wa tatu

Mwanamuziki huyo mkongwe ana watoto wawili kutokana ndoa yake ya kwanza.

Muhtasari

•Jumanne jioni, mwimbaji huyo ambaye sasa anaendesha mkahawa mjini Voi alichapisha picha inayomuonyesha kama kwamba ni mjamzito.

•Kwa sasa Nyota Ndogo yuko kwenye ndoa rasmi na mwanaume mzungu kutoka Denmark, Bw Henning Neilsen.

Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Mwanamuziki mkongwe kutoka Pwani, Mwanaisha Abdalla almaarufu Nyota Ndogo huenda kuwa anatarajia mtoto wake wa tatu.

Siku ya Jumanne jioni, msanii huyo ambaye sasa anaendesha mkahawa mjini Voi alichapisha picha inayomuonyesha kama kwamba ni mjamzito. Hata hivyo hakufichua maelezo yoyote zaidi katika sehemu ya maelezo na aliwaacha mashabiki kukisia tu.

Hata hivyo, wanamitandao ambao walitoa maoni chini ya chapisho lake, wakiwemo watu mashuhuri wenzake walionekana kushawishika kuwa kweli ni mjamzito huku wengi wao wakichukua hatua zaidi ya kumpongeza.

Tazama baadhi ya maoni;

Wahukagwi: Hongera sana mpenzi wangu.

Lill_fii: Hongera sana

Millychebby: Hongera

Fatma_unbreakable: Ma Sha Allah hongera sana

celestinegachuhi: Hongera

Nyota Ndogo tayari ni mama wa watoto wawili, mmoja wa kiume na mwingine wa kike, ambao alipata na aliyekuwa mume wake. Kwa sasa yuko kwenye ndoa rasmi na mwanaume mzungu kutoka Denmark, Bw Henning Neilsen.

Mwaka jana, mwimbaji huyo wa kibao 'Watu na Viatu' alifichua kuwa alikutana na mpenzi wake  Henning Nielsen nchini Marekani.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, alisemakuwa aliishia kuchumbiana na mzungu baada ya kutoridhishwa na mahusiano yake na wanaume wa Kiafrika.

Pia ameweka wazi kuwa hakujitosa kwenye mahusiano na raia huyo wa Udenmarki ili kujinufaisha kifedha ila ni kwa minajili ya kutosheleza kiu cha mahaba.

"Mimi niliteseka sana na Waafrika. Sio kuteseka umaskini lakini mapenzi. Hapa ndio nimepata mapenzi pesa mbona natafuta mwenyewe," Nyota alisema.

Nyota Ndogo na Bw Neilsen wamekuwa kwa ndoa kwa takriban miaka tisa. Ingawa wawili hao hawaishi pamoja, raia huyo wa Denmark amekuwa akimtembelea Nyota humu nchini mara kwa mara.

Hapo awali mwanamuziki huyo kutoka Pwani alikuwa kwenye ndoa nyingine ambayo ilikosa kufua dafu. Ana watoto wawili kutokana ndoa yake ya kwanza.