Mrembo afunga ndoa na baba mkwe baada ya mume mtarajiwa kutoweka siku ya harusi

Wisto Ahmad, kakake bi harusi alizungumza na waandishi wa habari kueleza kwa nini walikubali dada yao kuolewa na baba mkwe wake badala ya bwana harusi ambaye hakujulikana aliko.

Muhtasari

• Inaripotiwa kwamba takriban rupiah milioni 25 (shilingi elfu 250 za Kenya) zilikuwa zimezama kwenye hafla ya harusi.

Kisa cha kushangaza kiliripotiwa nchini Indonesia mapema wiki jana na kuzua minong’ono mitandaoni baada ya bibi harusi mtarajiwa kudaiwa kufunga harusi na baba mkwe baada ya kugundua kwamba bwana harusi mtarajiwa alikuwa ameingia mitini siku ya harusi.

Kwa mujibu wa video ambayo ilienezwa mitandaoni kutoka kwa hafla hiyo ya harusi, mwanamke huyo ambaye alitambulikwa na vyombo vya habari nchini humo kama SA alikuwa anatarajiwa kufunga pingu za maisha na mpenzi wake wa muda mrefu.

Siku ya harusi ilitakiwa kuwa siku yake ya furaha zaidi na aliisubiri kwa hamu sana kabla ya tukio la kutoweka kwa bwana harusi kutia kitumbua chao mchangani.

Wakati akitafakari pamoja na familia yake kuwaeleza wageni na wapendwa wake kwamba hawakuwa na chaguo ila kusitisha tukio hilo, baba mkwe wake, akiangalia pesa ambazo tayari zimeingia katika upangaji na utayarishaji wa hafla ya harusi, aliamua kuingilia ili kuokoa siku.

Wisto Ahmad, kakake bi harusi alizungumza na waandishi wa habari kueleza kwa nini walikubali dada yao kuolewa na baba mkwe wake badala ya bwana harusi ambaye hakujulikana aliko.

“Wageni walikuwa tayari wamefika kuhudhuria harusi hiyo. Familia ya mwanamume huyo ilitufahamisha kwamba mwana wao hayupo na hakuweza kupatikana,” alinukuliwa na odditycentral.com kusema.

Inaripotiwa kwamba takriban rupiah milioni 25 (shilingi elfu 250 za Kenya) zilikuwa zimezama kwenye hafla ya harusi, kwa hivyo kuifuta itakuwa uamuzi mgumu sana.

Katika video hiyo japo walikuwa wanaelezea kwa lugha ya kigeni, Baba wa bwana harusi na bibi harusi wanaonekana wakishiriki katika sherehe hiyo isiyo ya kawaida ya harusi katika video ambayo imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ya Indonesia, huku mmoja wao akijaza nafasi ya bwana harusi.