Harmonize afichua aina ya mwanamke atakayeoa huku akimshambulia vibaya Kajala

Staa huyo alibainisha kuwa yuko tayari kutulia katika ndoa na staa wa kike ambaye anaangaziwa sana kama yeye.

Muhtasari

•Alijigamba kuwa watu au vitu vinasikika tu wakati yeye mwenyewe anavizungumzia na vinasahaulika mara moja pindi anapoacha.

•Katika taarifa hiyo, staa huyo wa bongo fleva alisema imefika wakati anapoacha kuongelea kitu kinasahaulika kabisa.

Harmonize na aliyekuwa mpenzi wake Kajala
Image: HISANI

Bosi wa Konde Music Worldwide Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amesema ataoa tu mwanamke anayeendana na vigezo vyake.

Katika kile kilichoonekana kama kauli ya kumshambulia mpenzi wake wa zamani Frida Kajala Masanja siku ya Jumapili, mwimbaji huyo wa kibao ‘Single Again’ alidokeza kuwa yuko tayari kutulia kwenye ndoa na staa wa kike ambaye anaangaziwa sana kama yeye.

Alijigamba kuwa watu au vitu vinasikika tu wakati yeye mwenyewe anavizungumzia na vinasahaulika mara moja pindi anapoacha.

“Nina hakika unajua vitu vingapi au wau wangapi nilio acha kuwazungumzia huwaskii tena na unajua watu wangapi unawajua kupitia mimi!!! Star wakike mwenye dhamana kama vyangu ndio naweza kufunga naye ndoa,” Harmonize alisema kupitia Instagram.

Katika taarifa hiyo, staa huyo wa bongo fleva alisema imefika wakati anapoacha kuongelea kitu kinasahaulika kabisa.

“Mungu amenipa hiyo nguvu na ninajua!! Ukitaka kujua jiulize kipi kilichofanywa hilo kwenye nchi hii nisita au nisihusishwe, ujue hakihitaji nguvu kubwa,” alisema.

Kauli hiyo ya Konde Boy ilionekana kuwa ni shambulio lisilo la moja kwa moja kwa aliyekuwa mpenzi wake, muigizaji Kajala Masanja ambaye alihusika naye katika vita vya maneno takriban mwezi mmoja uliopita.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Mwezi uliopita, wapenzi hao wawili wa zamani waliotengana Desemba mwaka jana baada ya kuchumbiana kwa miezi michache walirushiana maneno makali kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Vita vilianza baada ya Kajala kufanya mahojiano na waandishi wa habari ambapo alijibu maswali mbalimbali kuhusu uhusiano wao uliovunjika ambao uligonga mwamba ghafla kuelekea mwishoni mwa mwaka jana.

Katika mahojiano hayo, muigizaji huyo mkongwe alimuagiza Harmonize kujitokeza waziwazi na kuweka mambo wazi iwapo alimsaliti kimapenzi katika kipindi cha miezi kadhaa ambayo walichumbiana mwaka jana. Alitoa agizo hilo wakati akijibu madai kuwa bosi huyo wa Konde Music Worldwide aliwahi kumfumania akimsaliti kimapenzi na mwanaume mwingine baada ya kupitia simu yake.

Kajala alimtaka staa huyo wa bongo fleva wakati kuweka mambo wazi wakati akilewa kama alivyokuwa ameapa.

“Aje aseme kama alinifumania ama nilimcheat aseme. Kama aliweza kuandika vitu vingine aseme,” Kajala alisema.

Baada ya kikao cha Kajala na wanahabari,Harmonize alidokeza amejikita katika kulewa na kumshambulia mpenziwe huyo wa zamani.

Katika taarifa yake ndefu kwenye Instagram, Konde Boy kwa jeuri alimtaka muigizaji huyo mkongwe kuacha kugombana naye kwenye mitandao ya kijamii na badala yake atafute mwanaume wa kumuoa.

Aidha, alidokeza kuwa haijulikani ni kwa nini mama huyo wa binti mmoja bado hajaolewa licha ya umri wake mkubwa.

“Tafuta bwana mzee mwenzio hata mganga kienyeji aliyezeeka zeheka. Acha kubishana na watoto online na kujitia moyo!! Usikute anajua anaweza kukutana na bang la take me back tena!! Kinachomfanya asiolewe hatukijuwi, kazi ni kumfwata fwata binti tuu!! Ukweli unaujua wewe!!” Harmonize alifoka.