Nilishambuliwa kwa maneno kwa kuwa 'mjamzito'- Janet Mbugua afunguka

Mbugua alifichua kabla ya hafla ya Mabingwa wa Kimataifa wa Jinsia ambapo alichaguliwa kuwa Msemaji Mkuu

Muhtasari

•Mbugua ambaye alikuwa anatarajia mtoto wake wa kwanza alisema watumiaji wa mitandao ya kijamii walimshambulia kwa kuwa mjamzito  na hakuelewa ni kwa nini.

Aliyekuwa mtangazaji wa Citizen TV Janet Mbugua amefunguka kuhusu changamoto alizopitia alipokuwa akifanya kazi kwenye runinga, akiwa na ujauzito wake wa kwanza.

  Mbugua ambaye alikuwa anatarajia mtoto wake wa kwanza alisema watumiaji wa mitandao ya kijamii walimshambulia kwa kuwa mjamzito  na hakuelewa ni kwa nini.

"Mwaka wa 2015 nikiwa Mtangazaji wa Habari kwenye Citizen TV, na nikiwa na ujauzito wa mzaliwa wangu wa kwanza,  nilishambuliwa mtandaoni, nikiwa na uhasama mwingi kwangu kwa kuwa na mimba".Alisema

Mbugua aliendelea kusema wengi wa wavamizi wake walimtaka kukoma kusoma habari hizo na kuchukua mapumziko hadi baada ya likizo yake ya ujauzito.

Hata hivyo hakukubali mashambulizi, Mtangazaji huyo wa zamani wa habari alisema kuwa alikuwa na wasimamizi wakuu ambao walimuunga mkono katika mchakato mzima. "Maoni mengi yalikuwa yakinitaka nirudi kwenye habari baada ya likizo yangu ya uzazi...

Nilikuwana timu ya ajabu na mabosi wakuu ambao waliniunga mkono," Mbugua alisema.

Mama huyo wa watoto wawili alibainisha kuwa hii ni sehemu tu ya mashambulizi mengi ya wanawake kuhusu kujukumika kifamilia  yanayoendelea kukumbana nayo mtandaoni.

"Ilikuwa ni mfano mmoja kati ya mingi, ya ubaguzi wa kijinsia mtandaoni, ambayo mamilioni ya watu, lakini haswa wasichana na wanawake, wanaendelea kukabiliana nayo," alisema.

Mbugua alifichua kabla ya hafla ya Mabingwa wa Kimataifa wa Jinsia ambapo alichaguliwa kuwa Msemaji Mkuu. Miongoni mwa masuala ambayo alitakiwa kuyazungumzia ni kuongezeka kwa visa vya unyanyasaji mtandaoni.

Janet Mbugua alifanya kazi katika runinga ya Citizen kwa zaidi ya miaka mitano, kabla ya kuacha kuendesha wakfu wake wa Inua Dada.