Samidoh ajibu baada ya Prince Indah kupendekeza awe miongoni mwa polisi watakaopelekwa Haiti

Kando na uimbaji, Samidoh pia ni afisa wa Polisi wa Utawala.

Muhtasari

•Prince Indah alipendekeza jina la Samidoh lijumuishwe kwenye orodha ya maafisa ambao watapelekwa kwa misheni ya kulinda amani nchini Haiti.

•Wakati akijibu pendekezo hilo, Samidoh aliuliza swali la kejeli kuhusu ikiwa Haiti badala yake ingeletwa Kenya.

Samidoh katika sare ya polisi
Image: HISANI

Staa wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh alijibu kwa utani baada ya mwimbaji mwenzake, Prince Indah kupendekeza jina lake lijumuishwe kwenye orodha ya Maafisa wa Polisi wa Kenya watakaopelekwa kwa misheni ya kulinda amani nchini Haiti.

Katika moja ya posti zake za utangazaji wa shoo, Prince Indah aliweka picha ya Samidoh akiwa amevalia sare ya polisi na katika sehemu ya maelezo, akawauliza mashabiki ikiwa mwimbaji huyo wa Mugithi ambaye pia ni afisa wa polisi anafaa kupelekwa katika nchini hiyo ya Amerika Kaskazini ambayo imekumbwa na mizozo.

"Ama Samidoh aende tu Haiti," Prince Indah aliandika kwenye mtandao waFacebook na kwenda mbele kutangaza ambapo angekuwa akipiga shoo jioni hiyo.

Wakati akijibu pendekezo hilo, Samidoh aliuliza swali la kejeli kuhusu ikiwa Haiti badala yake ingeletwa Kenya.

“Hawawezi leta Haiti?” Samidoh alijibu.

Prince Indah alisema, "Balaa!"

Kando na uimbaji, Samidoh pia ni afisa wa polisi kitaaluma na amekuwa katika idara ya usalama ya nchi kwa miaka mingi hata kabla ya kuingia kwenye muziki wa kitaaluma.

Image: FACEBOOK// PRINCE INDAH

Mapema mwezi uliopita, mwanamuziki huyo alijibu kwa ukali baada ya shabiki kumtaka ajiuzulu kutoka kwa Huduma ya Polisi ya Kenya na kuangazia ziara zake za muziki.

Chini ya moja ya machapisho yake ya Facebook, shabiki alidai kuwa serikali inaendelea kumlipa ilhali yeye ni mtalii zaidi kuliko afisa wa polisi.

Kutokana na ziara zake nyingi za muziki duniani, mtumiaji huyo wa Facebook aliyejitambulisha  alimtaka mwimbaji huyo kujiuzulu kutoka kwa huduma ya polisi na kuacha nafasi hiyo kwa Wakenya wengine wenye mahitaji kujaza.

“Na serikali inakulipa kama polisi na we ni more than a tourist ,si uresign tu uachie needy kenyans hio nafasi ya polisi juu hautaki kutulinda.....ata mtalii hawatembeagi vile unatembea baana,” shabiki alitoa maoni.

Katika majibu yake, Samidoh alionekana kutotiwa wasiwasi na agizo la mtumiaji huyo wa Facebook.

“Sasa unataka kulia?” alijibu.

Mwaka jana, mwanamuziki huyo ambaye ni afisa wa Polisi wa Utawala alisema hajapata sababu ya kuacha kazi ya kulinda usalama licha ya mafanikio yake katika tasnia ya muziki. Mara nyingi yeye hushiriki picha na video zake akitumbuiza katika sehemu mbalimbali za dunia lakini si akitoa huduma za afisa wa polisi.

"Ninafanya kazi siku za wiki na inapohitajika pamoja na kipindi cha wikendi huwa nafanya muziki wangu, kama talanta nyingine yoyote katika huduma ya polisi," alisema katika mahojiana na Word Is.

Msanii huyo alisema alijitahidi sana kupata kazi hiyo.

"Umewahi kwenda kwenye zoezi la kuajiri polisi na kuona watu wasio na mashati wakichukuliwa kupitia shughuli mbalimbali?" alisema.

"Kuacha kazi uliyotafuta chini ya mazingira hayo ni uchungu sana."