Ex wangu alimuahidi mamangu angekuwa wa kwanza kubebwa kwenye gari lake - Pritty Vishy

Alisema mamake aliporejea Kenya mwaka jana hata hivyo alikuta ex huyo akiwa katika hali mbaya zaidi kuliko jinsi alivyomuacha.

Muhtasari

•Mrembo huyo mwenye umri wa miaka 22 alifichua kwamba mpenzi wake wa zamani aliwahi kuahidi angembeba mzazi wake kwenye gari lake.

•Alisema kuwa mpenzi huyo wake wa zamani aliapa kwamba mamake ndiye angekuwa mtu wa kwanza kufurahia kupanda gari ambalo angenunua.

Image: INSTAGRAM// PRITTY VISHY

Mtayarishaji wa maudhui maarufu wa Kenya, Purity Vishenwa almaarufu kama Pritty Vishy amefunguka kuhusu ahadi kubwa ambayo mpenzi wake wa zamani alimpa mama yake.

Katika chapisho kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumanne, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 22 alifichua kuwa mpenzi wake wa zamani ambaye hakutaja jina lake aliwahi kuahidi kwamba angembeba mzazi wake kwenye gari lake.

Alisema kuwa mpenzi huyo wake wa zamani aliapa kwamba mamake ndiye angekuwa mtu wa kwanza kufurahia kupanda gari ambalo angenunua.

“Nimekumbuka tu jinsi ex wangu alivyowahi kumuahidi mama yangu kwamba atambeba kwenye gari lake. Namaanisha, atakuwa mtu wa kwanza kubebwa kwenye gari hilo,” Pritty Vishy alisema.

Alisema kuwa mama yake aliporejea nchini Kenya mwaka jana hata hivyo alipigwa na butwaa kukuta kwamba mpenzi huyo wake wa zamani alikuwa katika hali mbaya zaidi kuliko jinsi alivyomuacha.

".. Ilikuwa tu kwa mama yangu kwenda Saudi na kurudi na kugundua kuwa nilipoachana naye, mambo yalibadilika kutoka mbaya hadi mbaya," alisema.

Mtayarishaji wa maudhui huyo hata hivyo hakufichua ni mpenzi gani wa zamani ambaye alikuwa akimzungumzia. Kundi la watumiaji wa mtandao hata hivyo wanahisi kuwa anazungumza kuhusu mwimbaji Stephen Odero almaarufu Stevo Simple Boy, kwa kuwa ndiye mpenzi wake pekee wa zamani ambaye anajulikana hadharani.

Vishy alitengana na Simple Boy mapema mwaka wa 2022, miezi michache tu baada ya mahusiano yao kujulikana hadharani.

Wawili hao hata hivyo ilidaiwa hawakuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi kwani Stevo Simple Boy alidaiwa kutaka kusubiri ndoa kabla ya kushiriki tendo la ndoa na mtumbuizaji huyo mwenye umri wa miaka 21.

Katika mahojiano ya mwaka jana, Stivo alidokeza kwamba alichumbiana na Pritty Vishy wakati bado akiwa na mke wake, Grace Atieno. Alisema alipima tabia za wawili hao kabla ya kuamua mke wa kuwa naye. 

"Ukiwa na wasichana wawili unaangalia ni nani ako na utu, na ni nani ako wema na unyenyekevu. Kwangu mimi, unyenyekevu na kuvumilia kwake zilifanya nikavutiwa kwake," alisema msanii huyo kutoka mtaa wa Kibera.

Mwaka uliopita, Pritty Vishy alikuwa amedokeza kuwa kwenye mahusiano na mcheza santuri, DJ Starvy. Baadaye hata hivyo ilibainika kuwa wawili hao walikuwa wanataniana tu na hawakuwa wapenzi.