Kasisi wa Kikatoliki awataka warembo kuwatongoza wanaume badala ya kusubiri kutongozwa (video)

“Vunja hiyo kanuni mwambie ‘kaka, nimegundua unaniangalia sana, najua unanipenda ila huna ujasiri wa kunitamkia’… hapo hapo jamaa ataanza kucheka akimeza maneno," Kasisi aliwapa warembo 'mwakenya'

Muhtasari

• Mtumishi wa Mungu anawashauri kina dada, haswa wenye umri wa miaka 35 kwenda juu kutosubiri kutongozwa kama kweli wanaamini wana nyota ya ndoa.

Father Olouwa
Father Olouwa
Image: Facebook

Kuhani mmoja wa kanisa katoliki nchini Nigeria amezua tafrani katika mitandao ya kijamii baada ya klipu kuibuka akihubiri kuhusu wasichana wanaotaka ndoa.

Mtumishi wa Mungu anawashauri kina dada, haswa wenye umri wa miaka 35 kwenda juu kutosubiri kutongozwa kama kweli wanaamini wana nyota ya ndoa.

Kasisi huyo kwa jina Oluowa aliwashauri kina dada hao kuvunja sheria na kanuni za kusubiri kutongozwa, na badala yake kuchukua jukumu la kuwatongoza wanaume ambao wanaona wanawafaa.

“Dadangu mpendwa, unangoja mwanamume akuje atoe posa kwako? Miaka 35, unangoja tu uko tayari…vunja hiyo kanuni! Ninasema hili bila mzaha, kama wewe ni mwanamke ambaye anaona kabisa anastahili kuwa katika ndoa, unajua unaweza ukawa mke mwema, na uko na miaka 35, ikitokea umeona mwanamume ambaye ana nia kwako lakini hana ujasiri wa kukuambia, vunja hiyo kanuni potofu na umfuate mwanamume huyo,” mchungaji huyo alishauri.

Alisema kwamba kuna wanaume wasiokuwa na ujasiri wa kumwambia mrembo anampenda na akawataka warembo wakishaona dalili kama hizo, moja kwa moja wala wasisubiri bali wawe wa kwanza kutamka kwa mwanamume huyo.

“Vunja hiyo kanuni mwambie ‘kaka, nimegundua unaniangalia sana, najua unanipenda ila huna ujasiri wa kunitamkia’… hapo hapo jamaa ataanza kucheka akimeza maneno, mwambie utaifanya kuwa kazi rahisi kwake, mwambie vigezo vyako vyema kwamba u hodari katika mapishi, nitakuwa mke mzuri, sitaangalia simu yako, sitakusumbua kichwa na nitakuwa mama mzuri kwa wanetu,” mchungaji alivujisha siri kabisa.