Harmonize hatimaye anyenyekea na kuomba radhi baada ya kudai Mungu ni mwanamke

Konde Boy amezungumzia jinsi talaka ya wazazi wake ilivyoathiri maoni na heshima yake kwa wanawake.

Muhtasari

•Ukosoaji ambao umekuja hata kutoka kwa viongozi wa kidini umeonekana kumfanya msanii huyo kujutia matamshi yake.

•Pia alikiri kwamba Mungu hawezi kulinganishwa na mtu yeyote au kitu chochote.

HARMONIZE
HARMONIZE
Image: HISANI

Staa wa Bongo, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ameonekana kujutia sana kauli zake za hivi majuzi kuhusu madai ya Mungu kuwa mwanamke.

Bosi huyo wa Konde Music Worldwide aliyasema hayo mapema mwezi huu na kuzua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii huku wengi wakionekana kumkosoa.

Ukosoaji huo ambao umekuja hata kutoka kwa viongozi wa kidini umeonekana kumfanya mwanamuziki huyo kujutia matamshi yake na kuomba msamaha hadharani kwenye mtandao wa Instagram.

“Nakili kwa Mola wangu yakwamba niliteleza. Mimi ni kiumbe dhaifu mbele yake kwa kuwa sikupata elimu tosha ya kujua yeye ni nani. Kama ilivyo kwa wanadamu wengine bila shaka wanajiuliza hili swali!! Kosa langu ni kuliweka hadharani. Ukizingatia mimi ni mtu ninayetazamiwa na kufatiwa kwa ukaribu na jamii,” alisema Harmonize.

Mwanamuziki huyo kutoka Tanzania aliendelea kuzungumzia jinsi talaka ya wazazi wake ilivyoathiri maoni na heshima yake kwa wanawake.

 “Huruma yangu kwa mwanamke na kufwatilia tangu kuzaliwa kwangu nilimuoana mwanamke akicheza nafasi kubwa sana. Baba yangu na mama yangu walitengana nikiwa na miaka miwili kwa sababu baba yangu alioa mke wa pili, dini yangu hivyo! Na siku zote baba yangu alikuwa anasisitiza kwamba yeye ndiye kanilea na sio mama yangu. Namshukuru sana kwa hilo hakika alijitoa sana. Namuhudumia kwa chochote nampenda, ninaumombea sana!! Lakini baadaye nilikuja kugundua aliyenilea ni mama yangu wa kambo!!

Subhana Llah, hii dunia haiwezekani bila mwanamke!! Haya na mengine yalinipelekea kusema yote niliyoyasema!! Nichukue hii nafasi kuwashukuru viongozi wa dini wote kwa kunipatia elimu. Kiukweli nimeridhika na inatosha,” alisema.

Staa huyo wa bongo fleva aliendelea kuwamwagia sifa kemkem viongozi wa dini kwa miongozo waliyompa, maombi yao na usaidizi ambao wamempa.

Pia alikiri kwamba Mungu hawezi kulinganishwa na mtu yeyote au kitu chochote.

“Niombeeni ndugu zangu katika imani. Mungu apokee toba yangu!! Nitakuwa napost kila dua nitakayoombewa kuionyesha dunia upendo mkubwa kutoka kwa viongozi wangu wa dini yangu!! Msiache kunipembea kwenye muziki huku,” alisema.