"Mungu nilifanya kustahili haya?" Bahati ajawa bashasha baada ya Gachagua kuhudhuria hafla yake

DP Gachagua alikuwa mgeni rasmi, jambo lililomfurahisha Bahati na kumfanya ajivunie sana mafanikio yake.

Muhtasari

•Wakenya mashuhuri wakiwemo wasanii, wanasiasa na wanahabari walikuwa miongoni mwa wageni waalikwa kwenye hafla hiyo.

•Bahati alimpongeza naibu rais kwa kuonyesha sapoti kwa tasnia ya ubunifu kwa kuhudhuria hafla hiyo.

kwenye hafla ya Bahati na Diana Marua mnamo Juni 6, 2024.
Naibu rais Rigathi Gachagua kwenye hafla ya Bahati na Diana Marua mnamo Juni 6, 2024.
Image: VICTOR IMBOTO

Siku ya Alhamisi usiku, wapenzi maarufu Bahati na Diana Marua waliandaa hafla ya kupendeza ya kuzindua Reality Show yao ‘The Bahati’s Empire’ ambayo itaonyeshwa kwenye Netflix.

Hafla hiyo ilifanyika katika Hoteli ya Westwood jijini Nairobi na Wakenya mashuhuri wakiwemo wasanii, wanasiasa na wanahabari walikuwa miongoni mwa wageni waalikwa. Naibu rais, Rigathi Gachagua alikuwa mgeni rasmi, jambo lililomfurahisha Bahati na kumfanya ajivunie sana mafanikio yake.

Katika taarifa yake baada ya tukio hilo, mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za Injili ambaye kwa sasa amejiunga na tasnia ya filamu alisherehekea maendeleo yake na kuwashukuru wageni wote waliojitokeza.

“Nimejiunga na tasnia ya Filamu kama Mtayarishaji na kazi yangu ya Kwanza inakuwa kipindi cha Kwanza cha Uhalisia cha Kenya kwenye Netflix. Mungu wangu, nimejawa na machozi sasa, sitawahi Kujiita yatima kwa sababu nina Baba wa Mbinguni 🙏,” Bahati alisema kupitia Instagram.

Mwimbaji huyo wa nyimbo za mapenzi alimpongeza naibu rais kwa kuonyesha sapoti kwa tasnia ya ubunifu kwa kuhudhuria hafla hiyo.

“Kwa Mgeni Wangu wa Heshima; H.E Naibu Rais. Asante kwa kuonyesha shauku na sapoti yako kwa tasnia ya Ubunifu ya Kenya. Bosi wangu hii ilikuwa kwa muda mfupi na kutengeneza muda kutokana na ratiba yako yenye shughuli nyingi ya Kuja na Kuidhinisha, Kuunga mkono na Kuzindua shoo hili pamoja nasi imenipa uwezo wa Kuendelea Kufanya Me. Asante sana Naibu Wa Rais,” alisema.

Bahati pia hakusahau kumsherehekea mkewe Diana Marua kwa jukumu lake muhimu katika kipindi chao cha Reality Show.

“Mwisho; kwa Mke Wangu @Diana_Marua Nataka Ujue kuwa Wewe ni Nyota⭐️ Wewe ndiye ambaye Mungu alinichagulia na Hongera kwa kuwa Mtayarishaji Mtendaji katika filamu hii.

Najua umeshiriki mengi kwenye kipindi hiki na siwezi kusubiri kuonyesha ulimwengu kwa nini sisi ni Watengenezaji Bora wa vipindi vya uhalisia kwenye Tv nchini Kenya…,” alisema.

Mamia ya watumiaji wa mtandao pia wamejitokeza kwa wingi kumpongeza mwimbaji huyo na mkewe kwa mafanikio yao makubwa.