Akothee afunguka kwa nini alilazimika kuolewa akiwa na miaka 14, jinsi ndoa ilivyovunjika

Akothee aliitaja ndoa yake ya kwanza na baba wa mabinti zake watatu, Bw Jared Okello kama mazoezi ya ndoa tu.

Muhtasari

•Akothee alifichua mumewe wa zamani alikuwa asafiri kuenda Marekani na njia pekee ambayo angemfuata huko ilikuwa kwanza kufunga ndoa rasmi naye.

•Akothee alidokeza kuwa ndoa yake na Bw Jared iligonga ukuta baada ya mzazi huyo mwenzake kumpenda mwanamke mwingine.

Mwanamuziki na mfanyibiashara Akothee
Mwanamuziki na mfanyibiashara Akothee
Image: Instagram//Akothee

Mwimbaji maarufu wa Kenya Akothee amesisitiza kuwa ameolewa mara moja tu, ndoa yake ya sasa na mzungu Denis ‘Omosh’ Shweizer.

Akizungumza katika mahojiano na Dr. Ofweneke, mama huyo wa watoto watano aliitaja ndoa yake ya kwanza na baba wa mabinti zake watatu, Jared Okello kama mazoezi ya ndoa tu.

Alibainisha kwamba alikuwa mdogo sana wakati alipoolewa mzazi huyo mwenzake na alijua kidogo sana kuhusu ndoa.

"Nilikuwa na umri wa miaka 14, nilijua nini? Msichana wa miaka 14 anajua nini kuhusu ndoa?" Akothee alihoji.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 aliendelea kueleza mazingira yaliyompelekea kufanya harusi na Bw Jared Okello.

Alifichua kwamba mume huyo wake wa zamani alikuwa asafiri kuenda nchini Marekani na njia pekee ambayo yeye na watoto wao wangemfuata huko ilikuwa kwanza kufunga ndoa rasmi naye.

"Ex wangu alikuwa akienda Bahamas na watu wa SDA. Alitaka kurudi kunichukua pamoja na watoto. Njia pekee ambayo angeniongeza kwenye orodha yake ya kusafiri, ni kwa sisi kufunga ndoa. Harusi yangu iligharimu shilingi 2,500,” alisema.

Mwanamuziki huyo aliweka wazi kuwa bajeti yao ya harusi ya 2,500 ilishughulikia kila kitu kilichofanyika ama kutumia siku hiyo.

Alidokeza kwamba ndoa yake na Bw Jared iligonga ukuta baada ya baba huyo wa binti zake watatu kumpenda mwanamke mwingine.

Baada ya kutengana na Bw Jared, mwimbaji huyo alielekea Mombasa ambako alinuia kujiingiza katika shughuli ya kumpa riziki.

"Siku zote nilitaka kuwa dereva wa teksi. Sikuwa na karatasi za kwenda kugonga mlango wa mtu, nilikuwa na karatasi za kidato cha 4 tu. (Bw Jared) Alikataa na hati zangu pamoja na kitambulisho changu. Nilipoenda Mombasa singeweza kupata kazi yoyote, hata kuwa mhudumu inahitaji kitambulisho,” Akothee alisimulia.

Ni wakati alipokuwa Mombasa ambapo alikutana na baba yake mtoto wake wa nne ambaye alizaa naye mtoto mvulana wake wa kwanza, Prince Ojwang.

Oktoba mwaka jana, Akothee alithibitisha kwamba ndoa yake na Bw Jared Otieno ilivunjwa rasmi mnamo Mei  22, 2011 baada ya kesi ya talaka kuwasilishwa mwaka wa 2007.

Hii ni baada ya kuwa kwenye ndoa halali  na Bw Jared kwa takriban miaka mitano.

"Hati za talaka ziliwasilishwa mnamo 2007, Amri ya Nisi (Kabisa). Kwa hivyo, ndoa hii ilivunjwa mnamo Mei 22, 2011 na Mahakama ya Juu," alisema.