Akothee afunguka kwa uchungu kuhusu mgawanyiko mkubwa katika familia yake uliomfanya ajitenge

"Nilituma mtu kuwaambia familia yangu kuwa mimi ni mtu wa serikali, Nikifa leo serikali itanizika," Akothee alifoka.

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto watano aliwashutumu ndugu zake kwa kutosimama naye licha ya kuwa amewasaidia wote.

•"Mazishi yangu yatakuwa makubwa kuliko harusi yangu, (wanafamilia) wasiwe na wasiwasi kuhusu mimi kurudi kwao,” Akothee alitangaza.

Akothee na wazazi wake mnamo siku ya harusi
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mjasiriamali wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee amekiri kwamba kuna mgawanyiko mkubwa katika familia yake.

Akizungumza katika mahojiano na Presenter Ali baada ya kurejea nchini siku ya Jumatano, mama huyo wa watoto watano aliwashutumu ndugu zake kwa kutosimama naye licha ya kuwa amewasaidia wote.

‘Nimesaidia familia yangu.Nilipopata umaarufu, familia yangu haikuwahi kujua mahali nilipokuwa na nilichokuwa nikifanya. Baada ya hapo niliwasaidia wote. Nikichapisha taarifa zangu za benki leo, mtagundua wanafamilia wangu wote wametabasamu hadi benki,” alisema.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 alimshutumu dada yake mdogo Cebbie Koks kwa kuwashawishi wanafamilia wengine dhidi yake.

Alidai kwamba kaka zake hawakuichukulia kwa uzito harusi yake iliyofanyika Aprili kwani Cebbie alidaiwa kuwashawishi wanafamilia wengine kwamba ilikuwa njama ya kuharibu harusi yake na wakili Steve Ogolla ambayo ilifanyika mwezi Desemba.

“Tulipotangaza harusi yangu, ndugu zangu waliichukulia kirahisi. Nadhani yeye (Cebbie) alishawishi kila mtu kuwa hakukuwa na harusi, kulingana na kile tulichosikia. Alisema kuwa hakukuwa na harusi na nilitaka tu kuharibu harusi yake,” Akothee alijali.

"Nilitaka tu watu waweke tarehe ili mambo yasiingiliane. Ilitokea ikawaingia wafamilia wangu na kuonekana kama nilitaka tu kuharibu. Haikua vizuri. Kila mtu aliniona kama mtu mbaya, kama tufaha mbaya. Kumbuka nilikuwa sababu ya kuunganisha kwa familia yangu. Nimekuwepo, nimewaelimisha. Nimewasaidia. Iliponijia, mambo yalibadilika,” aliongeza.

Akothee aliweka wazi kuwa kisa hicho kilimfanya aanze kujitenga na familia yake na kufikiria kuishi maisha yake mbali nao.

"Polepole nilianza kujitenga, nikijitambua mimi ni nani. Katika luo huwa wanakungoja siku ukifa, nilituma mtu kuwaambia familia yangu kuwa mimi ni mtu wa serikali, Nikifa leo serikali itanizika. Mimi si mtu mwingine yeyote tu. Mazishi yangu yatakuwa makubwa kuliko harusi yangu, wasiwe na wasiwasi kuhusu mimi kurudi kwao,” alisema.

Hata hivyo aliweka wazi kuwa ana uhusiano mzuri na babake ambaye alimtaja kama shabiki wake mkubwa.

Pia alifichua kuwa harusi yake na Omosh takriban miezimiwili iliyopita ilifufua uhusiano wake na mamake kwani alipata kumweleza kuhusu mzozo wake na familia.

“Harusi imenileta mimi na mama yangu karibu. Nilimweleza kwa nini sikuzungumza naye kwa miezi mitatu. Maana kila mtu aliniona kana kwamba naleta matatizo kwenye familia kumbe wao ndio wananiumiza,” alisema.

Akothee pia aliwashutumu ndugu zake kwa kujaribu kumzuia baba yao kuhudhuria harusi yake iliyofanyika Nairobi.

Anasisitiza kuwa yeyote anayehisi amewakosea katika familia ajitokeze na kumweleza alichofanya na pia kuwataka waliomkosea kuchukua hatua ya kwanza kuomba msamaha.