Akothee ajibu kuhusu kutoa pete yake huku wasiwasi kuhusu ndoa yake na Omosh ukiongezeka

Wasiwasi kuhusu hatima ya ndoa ya mwimbaji Akothee umeendelea kuongezeka miongoni mwa Wakenya.

Muhtasari

•Akothee amekuwa kimya kuhusu mume wake Omosh na wadadisi wamekuwa wakimsukuma  kujibu kuhusu aliko mzungu huyo kutoka Uswizi.

•Akothee ambaye alionekana kutolipenda swali hilo alijibu, "Ndiyo nilitoa, piga simu kwa polisi na uvae yako."

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Wasiwasi kuhusu ndoa ya mwimbaji Akothee umeendelea kuongezeka miongoni mwa Wakenya siku baada ya siku huku wengi wakiendelea kuuliza maswali kuhusu hatima ya muungano huo ambao awali ulioonekana kuwa mzuri.

Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, Akothee amekuwa kimya sana kuhusu mumewe Denis ‘Omosh’ Shweizer na wanamitandao wadadisi wamekuwa wakimsukuma sana kujibu kuhusu aliko mzungu huyo kutoka Uswizi.

Siku ya Alhamisi, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alishiriki video akifurahia mlo mzuri na kama kawaida, kwenye sehemu za maoni, wanamitandao walimiminika na kila aina ya maswali na maoni haswa kuhusiana na ndoa yake. Mmoja wa wanamitandao waliotoa maoni alidai kuwa huenda mwimbaji huyo alivua pete yake ya ndoa na kumtaka ajibu.

“Kwani Akothee alitoa pete ya ndoa? Nauliza wakwe za Insta,” @janet_williams0 alimuuliza mwimbaji huyo kwenye Instagram.

Akothee ambaye alionekana kutolipenda swali hilo alijibu, "Ndiyo nilitoa, piga simu kwa polisi na uvae yako."

Uchunguzi wa karibu wa video ambayo mwanamuziki huyo alichapisha hata hivyo ulibaini kuwa ana pete mbili kwenye mkono wake wa kushoto. Sio wazi kama pete hizo ni zilezile alizowekwa kwenye kidole chake kuashiria ndoa.

Baadhi ya watumiaji wengine wa Instagram walimchokoza kwa kumuarifu jinsi wanavyommiss mzungu huyo ambaye alifunga naye ndoa mwezi Aprili.

Mmoja alibainisha jinsi mama huyo wa watoto watano amekuwa hamzungumzi Omosh hivi majuzi na kumfahamisha kwamba wanamtandao wanammiss.

“Siku hizi huongei stori za Omu-husband?? Tumem-miss,” @geogeousgal32 aliandika.

Akothee alimjibu, “Nenda umuoe ili usije ukamkosa.”

@ressymercy pia alitoa maoni, "Nimemiss Omosh."

Huku akimjibu, mwimbaji huyo alimwambia, "Miss mumeo, mpenzi wako au chochote, unamiss aje maisha ya mtu mwingine? Huna yako?"

Hivi majuzi, wanamitandao wamekuwa wakielezea wasiwasi wao kuhusu hatima ya ndoa ya Akothee na Omosh ambayo ilifungwa mnamo Aprili 10 mwaka huu.

Awali, wanandoa hao walionekana pamoja sana na hata kusherehekeana kwa maneno matamu ya mapenzi kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo halijaonekana tena kwa muda mrefu sasa, hali iliyowafanya wanamitandao kuibua wasiwasi na kuuliza maswali.