Akothee azungumzia madai ya kutengana na mumewe 'Omosh'

Kumekuwa na uvumi mwingi kuhusu ndoa ya Akothee na Omosh huku wengi wakidai wametengana.

Muhtasari

• Akothee alishangaa kwa nini watu wanadai kuwa ameachana na mume wake mzungu ilhali yeye mwenyewe bado hajasema.

•Akothee alitania kuwa harusi nyingine inakuja hivi karibuni akisema kuwa bwana harusi wake ajaye ataitwa ‘Bw Ojingo.’

Akothee na mume wake Denis Shweizer
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

MWIMBAJI Esther Akoth almaarufu Akothee amejibu madai yanayovuma kwenye mitandao ya kijamii kwamba ameachana na mumewe Denis ‘Omosh’ Shweizer.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alikuwa akishiriki mazungumzo na mtaalamu wa urembo Kristeen Kuria alipowazungumzia watu wanaodai kuwa ndoa yake imevunjika.

Katika video aliyoichapisha kwenye akaunti yake ya Instagram, Akothee alisikika akishangaa kwa nini watu wanadai kuwa ameachana na mume wake mzungu ilhali yeye mwenyewe bado hajasema.

“Na kwa nini wanadhani tumeachana? Ata sijasema tumeachana! Sijasema tumeachana na wameanza kuniambia ndio ‘Ojingo wa 8’,” alisikika Akothee akisema kwenye video hiyo.

Mama huyo wa watoto watano aliendelea kutania kuwa harusi nyingine inakuja hivi karibuni akisema kuwa bwana harusi wake ajaye ataitwa ‘Bw Ojingo.’

“Kuanzia leo, mimi ni Bi Ojingo. Ojingo ni jina la muda tukiwa bado tunamtafuta bwana harusi. Unapomwona tu bwana harusi anayefuata, ni ‘Ojingo’. Ita polisi," alisema.

Mwanamuziki huyo pia hakukosa kuwaonya watu wanaojifanya kumjali dhidi ya kumpigia simu wakitaka kujua zaidi akibainisja kwamba hana deni la maelezo kwa mtu yeyote nje ya safu yake ya watu wa karibu.

Uhusiano wa sasa wa Akothee na mumewe Denis Shweizer haujulikani wazi kwani bado hajatoa taarifa rasmi kuhusu hali ya ndoa yao. Hata hivyo, kumekuwa na tetesi nyingi kwamba ndoa hiyo haipo tena na kwamba hawako katika maelewano mazuri.

Vitendo vya hivi majuzi kwenye mitandao ya kijamii vimezidisha tetesi za kuachana huku wanamtandao wakiwa na shauku kubwa ya kupata majibu.

Baadhi ya mambo ambayo yamewaacha watu wakizungumza ni Akothee kukiri hajakuwa sawa kisaikolojia katika miezi michache iliyopita, mwimbaji huyo kuacha kujitambulisha kama  ‘Bi Omosh’ kwenye Instagram na akaunti ya Omosh kuzimwa.

Akaunti ya Instagram ya Mister Omosh ilizimwa siku ya Jumatatu na kuzidisha uvumi kwamba kunaweza kuwa na matatizo fulani ambayo bado hayajafichuliwa. Akaunti hiyo ilikuwa na takriban wafuasi 72,000 kabla ya kutoweka. Hata hivyo, haijulikani ikiwa akaunti imezimwa kwa muda au kabisa.

Akothee tayari alikuwa ameacha kufollow akaunti hiyo kabla haijazimwa na pia alikuwa amefuta picha kadhaa za mume huyo wake mzungu.Mama huyo wa watoto watano pia alikuwa amefanya mabadiliko kadhaa kwenye akaunti yake ya Instagram, akiondoa jina 'Mrs Omosh' kutoka kwa wasifu wake.