Akothee azungumzia sababu kuu ya kutohudhuria harusi ya dadake mdogo licha ya kualikwa, ugomvi wao

Mwimbaji huyo amekiri kuwa hakuhudhuria harusi hiyo kwani kulikuwa na tofuati kati yake na dada yake.

Muhtasari

•Akothee amekiri kuwa dada yake mdogo Cebbie Koks alimpigia simu kumfahamisha kuhusu harusi yake iliyofanyika Desemba.

•Akothee aliweka wazi kwamba hakuwa na tatizo lolte na harusi ya dadake, na kusema hata aliiunga mkono.

katika picha ya maktaba.
Cebbie Koks na dadake mkubwa Akothee katika picha ya maktaba.
Image: INSTAGRAM//

Mwimbaji Esther Akoth almaarufu Akothee amekiri kuwa dada yake mdogo Cebbie Koks alimpigia simu kumfahamisha kuhusu harusi yake iliyofanyika Desemba.

Cebbie alifunga pingu za maisha na wakili Steve Ogolla katika harusi ya kitamaduni iliyofanyika Rongo mnamo Desemba 28, 2022. Wanafamilia, marafiki na watu wengine wa karibu walihudhuria hafla hiyo nzuri lakini Akothee hakuonekana.

Akizungumza katika mahojiano na Presenter Ali, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alikiri kuwa hakuhudhuria harusi hiyo kwani kulikuwa na tofuati kati yake na dadake.

“Yeye ndiye amekuwa akivuka mipaka yangu na nimekuwa nikisubiri aje kuniomba msamaha jambo ambalo halifanyiki. Hakukuwa na jinsi ningeweza kujipeleka kwenye meza ambayo sikualikwa. Ni ukweli kwamba wakati mmoja alinipigia simu na kuniambia kwamba alitaka nije kwenye harusi yake, lakini hatukumaliza tofauti zetu. Hatukuwahi kuwa karibu zaidi,” Akothee alisimulia.

Mama huyo wa watoto watano alidokeza kuwa licha ya kutohudhuria harusi hiyo, aliunga mkono hafla hiyo kwa namna fulani kwani aliwaruhusu watoto wake kuwepo na hata kugharamia matumizi yao kwa siku hiyo.

"Harusi yake ilikuja. Niliwaachilia watoto wangu na kuwasapoti. Nililipia ndege yao. Oyoo na Ojwang walitaka kuwepo lakini nguo zao hazikufiki viwango. Nililipa karibu Ksh 45,000 kwa nguo za Ojwang na Oyoo zikiwemo za mume wangu.

Nilikuwa nikingoja dada yangu aje kunieleza na kusema samahani ili tuweke tofauti zetu nyuma. Lilikuwa ni neno pekee nililokuwa nikingojea kutoka kwake. Nilitaka atambue kuwa aliniumiza sana na nilichohitaji ni yeye kutambua na kusema samahani. Ingeishia hapo,” alisema.

Akothee aliweka wazi kwamba hakuwa na tatizo lolte na harusi ya dadake, na kusema hata aliiunga mkono. Hata hivyo alikiri kuwa tofauti zake na mdogo huyo wake zilimfanya asijitokeze katika hafla hiyo.

"Niliunga mkono kadri nilivyoweza. Nililipia tikiti za ndege kwa watoto wangu, nikawapa gari langu, walirudi nyumbani kwa kuchelewa, nikawapikia. Inaonyesha kuwa sikuwa na tatizo na harusi, kuna tatizo kati yetu ambalo lilikuwa halijapatiwa ufumbuzi na lilihitaji kutatuliwa. Ningewezaje kujialika huko?” Akothee alisema.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alimshutumu Cebbie kwa kuwashawishi wanafamilia wengine kumgeuka, jambo ambalo limemfanya ajitenge nao.

Takriban miezi 4 baada ya harusi ya dadake, Akothee pia alifunga ndoa na mpenzi wa maisha yake, Denis Shweizer almaarufu Omosh katika harusi nzuri iliyofanyika Nairobi mnamo Aprili 10.

Katika mahojiano, alifichua kuwa awali Omosh alikuwa amepanga kupeleka mahari mnamo Desemba lakini akamwomba amsubiri kwani dadake alikuwa akifanya harusi.

 “Tulipotangaza harusi yangu, dada yangu mdogo alikuwa akifanya harusi pia. Omosh alitaka kuleta ng’ombe Desemba na nikamwambia ashikilie kwa sababu Desemba tulikuwa tukifanya harusi nyingine,” alisema.

Cebbie pia hakuhudhuria harusi ya Akothee mnwezi Aprili na jambo hilo lilizua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu ugomvi wao wa kifamilia.