Bahati amfariji Diana kwa mapenzi baada ya kushambuliwa, azungumzia mipango ya harusi

Katika taarifa ndefu kwa mkewe, Bahati alimhakikishia mlibwende huyo kuwa yeye ni staa na ndiyo maana amekuwa gumzo.

Muhtasari

• Bahati aliweka wazi kuwa wakati mwingine huwa anajuta kumtambulisha Diana Marua kwenye macho ya umma kwani mara kadhaa amekuwa mwathirika wa upande mbaya wa umaarufu.

•Bahati alithibitisha kuwa mipango ya harusi yao bado iko na inakaribia kukamilika, akibainisha kuwa ana hamu kubwa ya kuweka pete ya ndoa kwenye kidole chake.

Diana Marua na mumewe Bahati
Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mwanamuziki wa Kenya Kelvin Kioko almaarufu Bahati alimwandikia mke wake Diana Marua ujumbe mzuri siku ya Jumanne jioni ili kumuonyesha upendo baada ya kushambuliwa vibaya na Wakenya kwenye mitandao ya kijamii.

Diana Marua amekuwa akivuma tangu mwisho wa juma lililopita huku baadhi ya Wakenya wakimshambulia kuhusu masuala mbalimbali katika maisha yake.

Katika taarifa ndefu kwa mkewe Jumanne jioni, Bahati alimhakikishia mlibwende huyo kuwa yeye ni staa na ndiyo maana amekuwa gumzo.

“Mpendwa Diana, najua umekuwa kwenye vichwa vya habari zinazotrend, najua kabisa haikusumbui ila nimeona nikukumbushe kitu kimoja kabla ya kulala. Wewe ni staa!!! Ningetamani ningekuwepo kukuambia hili Uso kwa Uso lakini niko nje ya jiji kwa mkutano wa Biashara, Nitarudi Nairobi Kesho,” Bahati alimwandikia mkewe kwenye Instagram.

Aliongeza, “Mke wangu; Unapendwa na Wengi, Unahamasisha Wengi, Unafuatwa na Wengi na kwa hayo mpenzi, huwezi kukosa chuki. Hakuna uwongo, umewapita wengi tangu nilipoandika post ya kwanza kukutambulisha kwa ulimwengu kama ‘Mshirika wangu wa maombi’.”

Mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili aliweka wazi kuwa wakati mwingine huwa anajuta kumtambulisha Diana kwenye macho ya umma kwani mara kadhaa amekuwa mwathirika wa upande mbaya wa umaarufu.

Hata hivyo, alibainisha kuwa mkewe kujulikana hadharani pia kumemsaidia kujenga chapa yake, jambo ambalo anajivunia kama mume wake.

"Wakati fulani nataka kukuomba msamaha kwa kukuweka kwenye upande huu wa ulimwengu usio na huruma lakini ukiangalia mambo Babe; Huu ulikuwa ni Mpango wa Mungu, Uliumbwa kwa ajili ya hili!!! Angalia Namba zako!!! Umekuja juzi tu na sasa wewe ndiwe Mtayarishaji wa Maudhui anayefuatiliwa na Kufuatwa zaidi katika YouTube Afrika Mashariki. Labda nisiseme hivi mara za kutosha lakini mimi ni Mume mwenye Fahari... Nina furaha Kukuita mke,” alisema.

Wakati huo huo, mwanamuziki huyo alithibitisha kuwa mipango ya harusi yao bado iko na inakaribia kukamilika, akibainisha kuwa ana hamu kubwa ya kuweka pete ya ndoa kwenye kidole cha mama huyo wa watoto wake watatu.

“Siwezi Kusubiri Kuteka Ulimwengu pamoja nawe; Ndiyoo mipango ya harusi yetu imekamilika kwa 70% na siwezi kusubiri kukuoa. NAKUPENDA,” alisema.

Katika jibu lake, Diana alimhakikishia mumewe kwamba anampenda sana na alibainisha kuwa wana ndoto kubwa za kufikia pamoja.

“NIMEMISS USIKU ZETU, SIWEZI KUSUBIRI KUKUMBATIA KWA NGUVU KESHO, MFALME WANGU. NAKUPENDA,” alijibu.