Bahati ashtushwa na hotuba ya kihisia ya bintiye, “Hata ukifa ujue tu tunakupenda!”

"Asante kwa kunisaidia kuwa na afya njema na pia kuninunulia nguo, na asante kwa kuwa mwaminifu kwetu," Mueni alimwambia Bahati.

Muhtasari

•Mueni ambaye ni binti ya Bahati akiwa na mpenzi wake wa zamani Yvette Obura alimsifu mwimbaji huyo kwa kuwa baba mzuri.

•Mueni aliendelea kumweleza baba yake kwamba anapoendelea kuzeeka kuna uwezekano mkubwa wa yeye kufa.

Bahati na bintiye Mueni
Image: INSTAGRAM// BAHATI

Mwimbaji mashuhuri Kelvin Kioko almaarufu Bahati alishiriki kipande cha video ya binti yake Mueni Bahati akimtakia Kheri ya Siku ya Akina Baba.

Katika video hiyo iliyochapishwa kwenye mtandao wa Instagram, Mueni ambaye ni binti ya Bahati akiwa na mpenzi wake wa zamani Yvette Obura alimsifu mwimbaji huyo kwa kuwa baba mzuri.

Mrembo huyo mwenye umri wa miaka saba aliangazia baadhi ya mambo mazuri ambayo mzazi huyo wake amemfanyia yeye na ndugu zake wengine ikiwa ni pamoja na kuwanunulia nguo, kuwapa makazi mazuri na elimu.

“Kheri ya siku ya akina baba, asante kwa kutununulia nyumba nzuri, asante kwa kutupeleka shule nzuri ambayo walimu hawatupigi, asante kwa kunisaidia kuwa na afya njema na pia kuninunulia nguo, na asante kwa kuwa mwaminifu kwetu," Mueni alimwambia babake kwa kujiamini.

Malkia huyo mdogo alitangulia kumhakikishia Bahati kuhusu upendo wao mkubwa kwake kwa ujumbe wa kipekee ambao ulionekana kumwacha mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili katika hali ya mshtuko.

"Hata ukifa utajua tu kwamba tunakupenda," Mueni alisema.

Bahati ambaye alionekana kuingizwa wasiwasi na ujumbe huo alisema, "Lakini sifi, asante lakini mimi sifi."

Mueni aliendelea kumweleza baba yake kwamba anapoendelea kuzeeka kuna uwezekano mkubwa wa yeye kufa.

"Ukizeeka, utakufa pia," alisisitiza.

Bahati aliucheka tu ujumbe wa kipekee wa binti huyo wake wa kwanza na alikuwa na shauku ya kujua ni wapi alijifunza hotuba hiyo.

Mueni kwa unyenyekevu alifichua kuwa mwana wa kulea wa Bahati, Morgan Bahati ndiye aliyemfundisha.

Mueni ni mtoto wa kwanza wa Bahati ambaye alizaa na aliyekuwa mpenzi wake, Yvette Obura. Alizaliwa takriban miaka minane iliyopita kabla ya wazazi wake kutengana.

Licha ya kutengana na Yvette miaka mingi iliyopita, mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili ameendelea kushirikiana naye vizuri katika malezi. 

Mke wa Bahati, Diana Marua pia anaonekana kumkubali binti huyo wa kwanza wa mwimbaji huyo na pia anamsaidia katika malezi. Hata hivyo kumekuwa na madai ya ugomvi usiyojulikana kati ya Diana na Yvette.