Edday Nderitu athibitisha alimuacha Samidoh kwa aliyemtaka zaidi huku akipingana na Karen Nyamu

"Siko kwenye ndoa ya wake wengi, kama ilivyoelezwa nilimuacha mume kwa yeyote aliyemhitaji zaidi,” Edday alisema.

Muhtasari

•Edday Nderitu aliweka wazi kuwa alimuacha mumewe ili kuwa na mwanamke ambaye alionekana kumtaka zaidi.

•Edday alisema hajutii uamuzi wa kugura ndoa yake ya miaka mingi na akaweka wazi kuwa ameweza kuwalea watoto wake bila usaidizi wowote.

Edday Nderitu, Karen Nyamu, Samidoh
Image: HISANI

Punde baada ya mahojiano ya seneta Karen Nyamu akidai kuwa Samidoh na Edday Nderitu bado wako katika uhusiano mzuri na huwa wanazungumza kuchapishwa kwenye mtandao wa YouTube, mke wa kwanza wa mwimbaji huyo wa Mugithi amejitokeza kukanusha madai hayo.

Katika taarifa kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii siku ya Jumamosi asubuhi, mama huyo wa watoto watatu ambaye kwa sasa anafurahia muda na familia yake nchini Marekani alitaja madai ya Nyamu kuwa si sahihi.

Edday aliweka wazi kuwa alimuacha mumewe ili kuwa na mwanamke ambaye alionekana kumtaka zaidi.

"Wacha nifafanue mambo machache ambayo yalishirikiwa mtandaoni na sio sahihi. Siko kwenye ndoa ya wake wengi, kama ilivyoelezwa nilimuacha mume kwa yeyote aliyemhitaji zaidi,” Edday alisema kupitia Facebook.

Aliongeza, "Nilifanya uamuzi wa kujiondoa mimi na watoto wangu kutoka kwa mazingira hayo yenye sumu, haswa binti yangu kijana ambaye kwa bahati mbaya anapokea moja kwa moja tabia isiyoaminika iliyoonyeshwa."

Mama huyo wa watoto watatu alidokeza kuwa hajutii uamuzi wa kugura ndoa yake ya miaka mingi na akaweka wazi kuwa ameweza kuwalea watoto wake bila usaidizi wowote.

Pia alizungumzia madai ya Karen Nyamu kwamba yeye na watoto wake huwa wanawasiliana na mwimbaji Mugithi kwa simu.

"Kuhusu mawasiliano na simu za video, nitaachia hapo kwani baadhi ya watu wanaonekana kuwepo wakati hilo linafanyika lakini mimi sifahamu. Katika msimu huu mpya wa maisha yangu, sihitaji drama yoyote, nahitaji amani tu, natumai kipindi kijacho cha mfululizo huu jina langu litaachwa,” alisema.

Katika mahojiano na na Ala C kwenye kipindi cha Reke Ciume na Ene, seneta Karen Nyamu alifichua kuwa Edday ambaye kwa sasa anafurahia wakati na familia yake nchini Marekani bado huwa anawasiliana na Samidoh na akadai kwamba hawezi kwenda popote kwani muungano wao hauwezi kuvunjika kwa urahisi.

“Mambo mnayoyaona kwenye mitandao ya kijamii mtashangaa sana, kuna baadhi ya miungano imetoka mbali sana. Labda hajui kwamba haendi popote, lakini najua kwa sababu miungano mingine si rahisi kukatika,” alisema.

Nyamu alidokeza kuwa mpenzi wake Samidoh na mkewe wa kwanza wamechukua mapumziko lakini bado wako katika uhusiano mzuri.

“Huwa naskia wakiongea, wako sawa sio vile mnafikiria. Hata watoto wanaongea naye kupitia simu yake. Kwa ground hakutawahi haribika,” alisema.

Seneta huyo alisisitiza kuwa yeye si mharibifu na akadokeza kuwa kuna mambo makubwa yatajidhihirisha katika siku zijazo.